Na Mwandishi Wetu,
MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameridhia kuwa tarehe 23 Agosti ambayo
ni siku ya Sensa na Makazi ya Watu iwe ni siku ya mapumziko.
“Ninayo furaha kuwajulisha wajumbe wa kikao hiki kwamba Mheshimiwa
Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia tarehe 23 Agosti iwe ni siku ya mapumziko
ili Watanzania wawepo majumbani, waweze kuwapokea makarani wa sensa na
kutoa maelezo husika,” amesema na kuamsha shangwe ukumbini.
Waziri Mkuu ametoa tamko
hilo leo (Jumatano, Agosti 17, 2022) kwenye kikao cha saba cha Kamati Kuu
ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kilichofanyika ukumbi wa
Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema
kutokana na uamuzi huo wa Mheshimiwa Rais, anaamini zoezi la sensa ya watu na
makazi litaenda vizuri kama lilivyopangwa.
Mapema, Waziri Mkuu
alipokea vishikwambi 600 kutoka kwa Balozi wa Korea Kusini, Mhe. Kim Sun Pyo
vyenye thamani ya shilingi milioni 202. Pia alipokea fulana 1,759 zenye ujumbe
wa kuhamasisha sensa zenye thamani ya sh. milioni 20 kutoka kwa Mkuu wa Kitengo
cha Taasisi za Serikali wa Benki ya NMB, Bw. William Makoresho ambaye
alikabidhi kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa benki hiyo.
Wajumbe wa kikao hicho walijulishwa kwamba utafiti uliofanywa na
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) umebainisha kuwa uelewa wa wananchi kuhusu
zoezi zima la sensa umefikia asilimia 99 ikilinganishwa na asilimia 96 ya Juni,
2022.
0 Comments