FAMILIA YAISHI NJE KWA MWEZI MMOJA BAADA YA BABA KUUZA NYUMBA

 


Na Mwajabu Hoza, Kigoma

 

FAMILIA ya mzee Enock Malago ya Manispaa ya Kigoma Ujiji Mkoani Kigoma imelazimika kuishi nje kwa takribani mwezi kutokana na  agizo la mahakama kuwatoa katika nyumba mara baada ya baba wa familia kuuza nyumba hiyo wakati akiwa baa na kutohusisha wanafamilia.

 

Mwaka 2013 katika Baa ndogo iliyojulukana kwa jina la Ishimwe mtaa wa Mlole manispaa ya Kigoma ujiji inaelezwa baba wa familia Enock Malago aliuza nyumba kwa makubaliano ya shilingi million 21.

 

Mama wa familia Meriasiana Jeremia amesema makaratasi ya makubaliona ya uuzaji wa nyumba yanaeleza mzee kupokea fedha kwa awamu tatu ambayo jumla ni million 15.5 na kesi ya uuzaji wa nyumba hiyo imedumu kwa muda wote huo mpaka Agasti 17 walipotolewa ndani ya nyumba kwa agizo la mahakama.

 

Amesema wakati kesi ikiendelea alipouliza aliambiwa atahamia katika nyumba nyingine jambo ambalo si la kweli ambali katika taarifa zilizofikishwa mahakamani kwenye kesi inaonekana kuwepo kwa nyumba moja na sio mbili.

 

Ameiomba serikali kuingilia kati suala hilo ili waweze kurudishiwa nyumba yao ambayo bado anamiliki hati yake na kusema kuwa  mumewe alistaafu kazi na kwa sasa ni mlemavu anatembelea magongo. 


Enock Malago ambaye ni baba wa familia anaeleza sababu za kuuza nyumba bila ya kushirikisha mwenza wake ni mara baada ya kuona maisha ya mjini yamekuwa magumu kwake na hivyo kuhitaji kurudi kijijini.

  

Familia hiyo ina jumla ya Watoto sita na wakizungumza kwa niaba ya wenzao Neema Enock na Norbet Enock wameeleza kusikitishwa na Ushahidi uliofika mahakamani ambao unawataja baadhi ya watoto kushiriki katika mchakato wa uuzaji wa nyumba hiyo jambo ambalo wameeleza si kweli.

Post a Comment

0 Comments