TRA YAKAMATA MAROBOTA 600 YA VITENGE KUTOKA NJE YA NCHI YALIYOINGIA KIGOMA



Na Mwajabu Hoza, Kigoma.

MAMLAKA ya mapato Tanzania TRA mkoani Kigoma imekamata Marobota takribani 600 ya Vitenge yaliyokuwa yakiingizwa kimagendo mkoani humo kutokea nchini Congo DRC.

Marobota hayo ambayo yalikuwa yakisafirishwa kwa njia ya Boti yamekamatwa siku ya jana Katika kijiji cha Kabeba kata ya Mwakizega wilayani Uvinza yakiwa yamehifadhiwa katika  nyumba iliyo karibu na ufukwe wa Ziwa Tanganyika.  

Kaimu Meneja mamlaka ya mapato TRA mkoani Kigoma Deogratius Shuma ameeleza hadi sasa wamiliki hawajapatikana,thamani ya mzigo sanjari na kodi ambayo ingepotea kutokana na watu hao kuungiza mzigo huo kimagendo.

Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma Filemon Makungu ameeleza kutokana na mizingi hiyo kuandikwa majina tofauti tofauti upelelezi unaendelea ili kuwakamata wamiliki hao.

“Taarifa tunazo nani rahisi sana kuwakamata kama ambavyo tumeweza kukamata mizigo hii basin a wamiliki pia watakamatwa taratibu zinaendelea ili kuhakikisha watu wote wanakamatwa “ alisema Kamanda.            

Mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amefika katika kijiji cha Kabeba eneo ambalo bado mzigo unaendelea kupakiwa Katika magari tangu siku ya jana jion na kuwataka wafanyabiashara kuacha tabia ya kukwepa kodi.

Amesema lengo la serikali ni kuona wafanyabiashara wanakuwa kiuchumi na haiwezekani kukua kwa kufanya biashara za magendo hivyo warudi kwenye taratibu za serikali za kupitisha bidhaa nchini kwa njia ambazo ni halali na serikali iweze kuboresha mazingira ya wao kufanya biashara zao.

Baadhi ya wakazi  wa Kijiji cha Kabeba akiwemo Hussein Mustafa amesema tukio hilo ni kwa mara ya kwanza kuliona likitokea katika kijiji chao ambapo wao mara kadhaa wamekuwa wakisafirisha bidhaa ndogondogo kwenda mikoa jirani na sio nje ya nchi.

 


Post a Comment

0 Comments