WALIMU NA WANAFUNZI KUNUFAIKA NA ELIMU YA UJIFUNZAJI KUPITIA MBINU ZA MICHEZO

 


Na Mwajabu Hoza , Kigoma

MASHIRIKA sita yasiyo ya Kiserikali yanatekeleza mradi wa Play Matter katika Nchini tatu ikiwemo Tanzania, Ethiopia na Uganda na lengo ni  kutoa elimu kwa jamii, walimu na wanafunzi jinsi ya kutumia michezo katika ujifunzaji na ufundishaji elimu ya awali pamoja na shule za msingi.

Akizungumzia hilo Stephen Myamba mkuu wa IRC wilaya ya Kasulu amesema mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha mwaka 2020/2026 na  walengwa wa mradi ni watoto kuanzia umri wa miaka 3 hadi 12+.

Nchini Tanzania mradi unatekelezwa Kigoma na mashirika yanayosimamia mradi huo ni pamoja na shirika la International Rescue Committee (IRC) pamoja na Plan International na maeneo ya  utekelezaji wa mradi ni katika kata tatu ambazo ni Nyamidaho wilaya ya Kasulu pamoja na Rusohoko na Murungu wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.

Amesema mradi huo unatekelezwa katika kambi za wakimbizi ikiwemo Nduta wilayani Kibondo na Nyarugusu wilayani Kasulu na vijiji vinavyozunguka kambi hizo ambapo jumla ya watoto 100,000 wenye umri wa miaka 3 hadi 12+ watafikiwa na mradi huo.

“Huu mradi unalenga zaidi wakimbizi waliopo makambini ambapo watoto 65,009 sawa na asilimia 60 katika shule za wakimbizi na watoto 43,000 sawa na asilimia 40 kwa shule za msingi zilizopo vijiji jirani na kambi za wakimbizi kwa kibondo na Kasulu” alisema Myamba 

Wakitambulisha utekelezaji wa mradi huo kwa waandishi wa habari mkoa wa Kigoma wakati wa  semina elekezi ya siku moja Masunga Isumbi afisa mawasiliano IRC na Mratibu Msaidizi wa Elimu IRC Arip Kiriama  wamesema lengo ni kuhakikisha waandishi wanatambua vizuri utekelezaji wa mradi huo kwa Kigoma. 

Walisema waandishi wana nafasi kubwa ya kuutangaza mradi kwa wananchi ili wawe na uelewa sahihi kuwa watoto wanaweza kujifunza kupitia michezo na kuongeza uelewa wao zaidi katika kuwajenga kimwili, kihisia, kiafya na kijamii.

Katika jitihada za kuutangaza mradi walisema hadi sasa mradi umeshatambulishwa kwenye sekta muhimu ikiwemo wizara ya elimu, maendeleo ya jamii, vyombo vya habari wakiwemo wahariri lakini pia kutengeneza miongozo ya vitabu vinavyohusisha michezo mashuleni.

Miongozo hiyo itasambazwa kwa viongozi wa kijamii, wazazi, walezi  na viongozi wa dini ili kutoa dira na uelewa jinsi ya kutumia michezo kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia kwa watoto wao wakiwa nyumbani.

Donatus Mlelwa akizungumzia utekelezaji wa mradi huo amesema wamelenga kutoa elimu kwa walimu 1485 kwa shule 55 kutoka katika kambi za wakimbizi na walimu 426 kwa shule 45 kutoka katika vijiji vinavyozunguka makambi.

Amesema walimu watapewa mbinu na ujuzi wa namna ya kuandaa masomo yao ya darasani kwa kuhusisha michezo kwa watoto na lengo ni masomo hayo yawe shirikishi, yenye kufurahisha, kuvutia na kueleweka kwa watoto.

Ukiachia mbali kutoa elimu kwa walimu lakini pia mradi utajikita katika kuandaa mazingira ya ya kuchezea kwenye shule ambazo mradi unatekelezwa, kuboresha madarasa yanayozungumza na changamshi, pamoja na kutoa elimu kwa jamii umuhimu wa michezo kwa watoto.

“ Lengo kuhakikisha michezo inakuwa ni sehemu ya watoto kujifunza wakiwa shule lakini pia wakiwa nyumbani na itachochea uelewa mkubwa wa masomo kwa watoto , na tumeshaandaa miongozo ambayo itatumika kufundishia na ikumbukwe kuwa kufundisha mtoto kwa kumchapa sio sababu ya yeye kuelewa isipokuwa inamjengea uoga na nidhamu ya uoga pia.” alisema.

Akizungumza kwa upande wa waandishi wa habari Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Kigoma Deogratius Nsokolo amesema wanahabari wapo tayari kuungana na mashirika, asasi na serikali katika kuhakikisha jamii inapata taarifa mbalimbali zinazowahusu kwa maslahi yao.

“ Jukumu letu ni jamii kupata taarifa zilizo sahihi na zenye tija kwao hivyo mradi huu unatakiwa kuwa wa wazi kwa waandishi ili waweze kushiriki kuelimisha jamii kupitia vyombo vyao wanavyoandikia ikiwemo magazeti, Radio , Luninga, lakini pia kuna mitandao ya kijamii hii itachochea ujumbe kufika kwa haraka kwa wananchi kupitia vyombo hivyo” alisema .

Lakini pia serikali inaendelea kuboresha ushirikiano wa kisekta katika utoaji wa huduma za malezi jumuishi kwa watoto kupitia Programu ya kitaifa ya PJT-MMMAM yenye lengo la kuleta uchechemuzi wa malezi ya msingi ya watoto kupitia vipengele vitano ikiwemo afya, lishe, ulinzi na usalama, malezi yenye mwitikio na ujifunzaji na uchangamshaji wa awali wa mtoto katika umri wa kuanzia miaka 0 hadi 8.

Kwa mwaka wa bajeti 2021/22 hadi 2025/2026  ya program hiyo imetenga asilimia 24 kwa ajili ya utoaji wa elimu kwa jamii wakiwemo wazazi na walezi kuhusu vipengele vyote vya ukuaji na maendeleo ya mtoto na kuhususha michezo kama sehemu ya ukuaji wa ubongo wa mtoto.

Afisa elimu msingi Richard Mtauka kutoka Manispaa ya Kigoma Ujiji  amesema endapo muongozo utatolewa katika shule za msingi kufundisha masomo kupitia michezo itawawezesha watoto kuelewa kwa urahisi, kuwapa furaha lakini pia kupunguza utoro.

“Walimu wanaofundisha elimu ya awali wamekuwa wakifanya hivyo lakini kwa kusema madarasa yote yafundishwe masomo yao  kupitia michezo inahitajika elimu kwa walimu wetu wanaofundisha ili wapate mbinu na ujuzi wa kufundisha kwa kupitia michezo” alisema Mtauka

Baadhi ya wazazi wameeleza mfumo huo wa ufundishaji unaweza kuwa mgumu kwao kuelewa kama watoto wao wanaelewa vyema masomo ya darasani  lakini endapo walimu watapata elimu sahihi na kuelewa jinsi ya kuwafundisha watoto na wakaelewa basi hata wazazi pia wataelewa na kuona umuhimu wake.

 “Wazazi tulio wengi tunapenda kuona mtoto alichoandika shule bila kujali umri wake kwa kipindi hicho anatakiwa aanze kujifunza nini , tukiona mtoto kaandika na kasahihishiwa na mwalimu ndio tunaona kuwa mtoto kaenda shule kusoma na sio kucheza” Amesema.

Kwa  mujibu wa Sera ya elimu ya mwaka 2014 Serikali, kwa kushirikiana na wadau itatilia mkazo zaidi katika kuweka mazingira mazuri ikiwemo kuendelea kuboresha mitaala ya elimu na mafunzo ili ikidhi mahitaji ya maendeleo ya Taifa.

 

 

 

Post a Comment

0 Comments