WANANCHI WALALAMIKIA KUSHAMILI KWA UVUVI HARAMU ZIWA TANGANYIKA

 


Na Mwajabu Hoza, Kigoma.

WANANCHI katika Vijiji vya Herembe na Kaparamsenga Kata ya Herembe wilaya Uvinza mkoani Kigoma,  wamelalamikia kushamili kwa uvuvi haramu wa kutumia nyavu za Ringnet unaofanywa na wavuvi kutoka maeneo mengine huku uvuvi huo  ukiathiri  hifadhi na mazalia ya dagaa na samaki katika Ziwa Tanganyika.

Kauli hiyo imetolewa na wananchi wa kijiji hicho ambapo wameutuhumu uongozi wa kijiji akiwemo mwenyekiti wa kijiji hicho ambaye amekuwa chanzo cha ujio wa wavuvi  kutoka maeneo mengine na kufanya uvuvi haramu katika maeneo yao.

Mwenyekiti wa wavuvi Kijiji cha Kaparamsenga Biocheni Bidaha amesema dagaa zinazovuliwa ni ndogo ndogo na kuharibu mazalia ya mazao hayo huku Shabani Juma mkazi wa kijiji cha Herembe amesema serikali imeshapiga marufuku  uvuaji wa kutumia Ringnet ambazo zinavua hadi mazalia ya samaki. 

Konfrence Myeba ambaye ni Mwenyekiti kitongoji cha Kefu amesema eneo ambalo wavivu wengi wanafanya uvuvi haramu ni katika mwalo wa Kashe “Niliwakusanya wavuvi na wananchi tukaanza utaratibu wa kulinda maeneo yetu ili kuzuia matumizi ya nyavu haramu ” amesema  

Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha Herembe Fabian Batezi amepinga tuhuma hizo na kueleza kuwa hana taarifa za wavuvi ambao wanatumia Ringnet katika eneo lake na kueleza kuwa hajapewa taarifa za nyavu ya aina gani inapaswa kutumika katika shughuli za uvuvi na kwamba wamejiandaa kuchukua hatua kwa wavuvi haramu.

Akizungumzia hilo mkuu wa wilaya ya uvinza Hanafi Msabaha amesema uvuvi wa aina hiyo umeshamiri maeneo ya mwambao wa ziwa Tanganyika licha ya hatua kuchukuliwa  mara kwa mara.

Kutokana na hilo Msabaha amewaagiza maafisa uvuvi kufanya operation kubaini wavuvi haramu na kuwakamata mara moja kwa kushirikisha viongozi wa vijiji na hatua kali zichukuliwe dhidi yao.

“Zoezi hili liwe la mara kwa mara ili kukomesha Uvuvi haramu na wengine wamekuwa wakitumia uvuvi wa kokoro ambao unamaliza samaki wote na mazalia yaliyopo na kufanya masiha ya wananchi wa ukanda wa Ziwani kuwa na hali ngumu ya kiuchumi kwa kuwa shughuli yao kubwa ni uvuvi ” amesema  Mkuu wa wilaya Msabaha.

 

Post a Comment

0 Comments