Na
Mwandishi Wetu.
Serikali ya Jamhuri ya Korea imeipatia Tanzania mkopo
wa gharama nafuu wa shilingi bilioni 310 kwa ajili ya upanuzi wa mfumo wa
utambuzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na uendelezaji na
utunzaji wa mfumo wa taarifa za ardhi.
Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo baina ya
Serikali ya Tanzania na Korea Kusini itakayotolewa kupitia benki ya Exim ya
Korea, imefanyika leo (Alhamisi, Oktoba 27, 2022) katika ukumbi wa Ofisi ya
Waziri Mkuu wa Korea Kusini iliyopo Seoul.
Mkataba wa awamu ya pili ya mradi wa upanuzi wa mfumo
wa utambuzi wa NIDA una thamani ya shilingi bilioni 161 na mkataba wa
uendelezaji na utunzaji wa mfumo wa taarifa za ardhi ambao una thamani ya
shilingi bilioni 149.
Akizungumza wakati wa halfa hiyo ambayo pia ilishuhudiwa
na Waziri Mkuu wa Korea Han Duck-Soo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa
Tanzania na Korea zinajivunia mahusiano yaliyodumu kwa miaka 30 ambayo yamekuwa
chachu katika kukuza uchumi wa nchi hizo mbili katika sekta mbalimbali.
“Tunaishukuru sana Korea Kusini kwa kuwa miongoni mwa
mataifa yanayoshiriki katika kutatua changamoto za kimaendeleo ikiwemo kupitia
Mfuko wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Korea (EDCF)”
Amesema kuwa kupitia mfuko huo, Tanzania imeweza
kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo madaraja, barabara, kituo cha kisasa cha
kusajili meli cha Zanzibar, njia ya kusafirishia umeme, hospitali ya
Mloganzila, mradi wa umwagiliaji uliopo Zanzibar na utoaji huduma wa
vitambilisho vya Taifa. “Miradi hii yote imegharimu zaidi ya dola za Kimarekani
milioni 733.”
Waziri Mkuu amesema kuwa pamoja na mikopo kupitia
mfuko wa EDCF, Tanzania pia imekuwa mnufaika wa mikopo kupitia Shirika la
Maendeleo la Korea (KOICA). “Tunaishukuru sana Jamhuri ya Korea kwa kutambua
kuwa Tanzania ni nchi ya kipaumbele.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema misaada ya KOICA kwenye
eneo la afya, elimu ya ufundi, ufadhili wa masomo imesaidia sana kuleta nguvu
na msukumo katika kuongeza kasi ya maendeleo ndani ya Serikali.
Naye, Katibu Mkuu Wizara
ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba amesema kuwa mkataba wa awamu ya pili wa
mradi wa upanuzi wa mfumo wa utambuzi wa NIDA utaiwezesha mamlaka hiyo kuongeza
uwezo wa kutengeneza vitambulisho vya Taifa pamoja na kutunza takwimu. “Mkopo
huu utaisaidia NIDA kujikita katika maeneo ya vijijini na kuongeza kasi ya
usajili wa vitambulisho.”
Akiuzungumzia mkataba wa uendelezaji na utunzaji wa
mfumo wa taarifa za ardhi, Katibu Mkuu huyo amesema kuwa mkataba huo
utaiwezesha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa na mfumo mpya
wa kidijitali badala ya utunzaji wa kwenye makaratasi.
“Tunaamini utaratibu huu mpya utaleta urahisi na
utaondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zinatokana na kutokuwepo kwa mfumo
rahisi na mzuri wa uhifadhi wa taarifa.”
Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na
Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi
Mbarouk Nassor Mbarouk, Balozi wa Tanzania Nchini Korea Kusini, Balozi Togolani
Mavura, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Aboud Hassan
Mwinyi na watendaji wengine wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
0 Comments