RAIS SAMIA: SERIKALI ITAENDELEA KUBORESHA VITUO VYA AFYA NCHINI

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Samia Suluhu Hasan akizindua hospitali ya wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma

Na Mwajabu Hoza, Kigoma 

RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan  amesema serikali itahakikisha inaendelea kuboresha huduma za afya nchini ikiwemo kuweka vifaa tiba ili kuwasaidia wananchi kuondoa changamoto kufuata huduma hizo maeneo ya mbali.

Ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake mkoani Kigoma ambayo imeenza jana wilayani Kakonko ambapo amezindua hospitali ya wilaya ya wilaya hiyo ambayo ujenzi wake umegharimu takribani bilioni 3.5 ikiwemo na vifaa tiba.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Samia Suluhu Hasan akisikiliza maelekezo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Tobias Andengenye baada ya kuzindua hospitali ya wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma

Amesema ujenzi wa hospitali hiyo unalenga kuwaondolea wananchi vikwazo vya upataji wa huduma bora "hii hospitali ni yenu jitahidini kutunza mali yenu kituo chenu kiweze kuwahudumia leo na kesho na serikali itaendelea kuleta vifaa ambavyo havipo kwa ajili yenu wananchi" Alisema Rais

Sanjari na hilo Raisi Samia amezindua mradi wa maji katika eneo la Kanyamfisi wenye dhamani ya zaidi ya shilingi bilioni 4 mradi ambao utahudumia Kata nne za wilaya ya Kakonko pamoja na mradi wa barabara ya Kabingo hadi Nyakanazi yenye urefu wa kilomita 50 kwa kiwango cha lami kwa dhamani ya shilingi bilioni 43.  

Raisi Samia Suluhu Hassan amesema miradi hiyo itachochea ukuaji wa maendeleo ya wananchi hivyo watumie miradi hiyo kama fursa ya ukuaji wao wa kiuchumi ikiwemo kuanzisha miradi mbalimbali yenye tija.

Akihitimisha Ziara yake kwa wilaya ya Kakonko na Kibondo Rais Samia amefanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Umoja na kuzungumza na wananchi ambapo amesema serikali itaendelea kuboresha huduma za kimaendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya ,Maji , Umeme, Barabara na elimu.

Wananchi wa wilaya hizo wametoa shukrani zao kwa serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo afya elimu na miundombinu ya barabara miradi ambayo inatoa fursa ya ukuaji wa maendeleo kwenye wilaya zao.

Ziara ya siku nne yaRaisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza jana katika wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma ambapo inatarajiwa kuhitimishwa ndani Manispaa ya Kigoma Ujiji Mkoani Kigoma na lengo ni kukagua, kuweka jiwe la msingi, kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.

 

Post a Comment

0 Comments