TANZANIA NA DRC ZASAINI HATI YA MAKUBALIANO

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 23 Oktoba, 2022.

Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo wameshuhudia utiaji saini hati ya makubaliano (MOU) inayohusu ushirikiano katika masuala ya teknolojia (ICT), Posta na Mawasiliano baina ya nchi hizo.

Zoezi hilo lilifanyika, Ikulu Jijini Dar es Salaam hapo jana Oktoba23, 2022 ambapo kwa upande wa Tanzania, Mkataba huo umesainiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye na kwa upande wa DRC umewekwa saini na  Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya nje wa DRC, Mhe. Christophe Lutundula.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye (Kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC  Christophe Lutundula, wakisaini hati ya makubaliano baina ya nchini hizo huku wakishuhudiwa na Marais wa nchi hizo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais, Ikulu,  Tanzania na DRC zimekubaliana kushirikiana na kuendeleza sekta ya mawasiliano kwa kuwa ni sekta pekee inayozalisha rasilimali pamoja na ajira kwa vijana kwa kiasi kikubwa.

Aidha katika kukuza jitihada za biashara kati ya nchi hizo mbili, Rais Samia alisema serikali ya Tanzania inaifanyia marekebisho meli ya MV Sangara ili ianze tena kutoa huduma ya kusafirisha mizigo kati ya Tanzania na DRC.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 23 Oktoba, 2022.

Aliongeza kuwa Tanzania na DRC kwa kushirikiana na Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) zina mpango wa kujenga ushoroba wa kati (Central Corridor) wa barabara itakayounganisha Tanzania na DRC.

Takwimu za biashara baina ya nchi hizo mbili zimepungua kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, hivyo nchi hizo zimefufua Tume ya pamoja ya Ushirikiano ili kukuza uhusiano na ushirikiano uliopo kwa manufaa ya nchi zote mbili.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo, akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 23 Oktoba, 2022.


Post a Comment

0 Comments