WAMILIKI WA MABOTI KIGOMA WAIOMBA SERIKALI KUKABILIANA NA UGONJWA WA EBORA

 


Na Mwajabu Hoza , Kigoma

UMOJA wa wamiliki na wasifirishaji wa maboti Mkoani Kigoma UWAMAKI  wameomba serikali kuwa na mkakati wa kikabiliana na  maambukizi ya ugonjwa wa Ebola kwa kuwa na vifaa vya kisasa vya kupima ugonjwa huo ambavyo vitasaidia kubaini wagonjwa wenye dalili na kuepusha watu wengi kukaa karantini wakisubiri hatma yao kwa muda mrefu.

Mweyekiti wa umoja huo Kashindi Adam amesema eneo la Kibiriza ambapo wageni kutoka nchi za Congo DRC na Burundi huingia na kutoka nchini, vipimo vinavyotumika ni vile vya kupima joto la mwili pekee na kudai inaweza kusababisha watu wengi ambao hawana maambukizi hayo kuweka karantini.

“Tunaiomba serikali iweze kutupatia vifaa vya kisasa ambavyo vitatumiwa na wahudumu wa afya waliopo katika eneo letu la kibirizi kuwapima wasafiri wanaoingia na kutoka ili kama ikibainika mtu ana ugonjwa huo serikali iweze kuchukua hatua za haraka” amesema

Mganga mkuu wa mkoa wa Kigoma Dokta Jesca Lebba amesema idara ya afya imeweka mikakati yote ya kuhakikisha wageni wanaongia nchini wanafanyiwa vipimo na wale wenye dalili kutengwa sehemu maalumu ambazo tayari zimeandaliwa.

Amesema  hatua zingine zilizochukuliwa ni pamoja na kuwaagiza wahudumu ngazi ya jamii kutoa elimu juu ya dalili, jinsi ya kujikinga na wapi watu wanaweza patiwa msaada pindi wanapokuwa na mtu mwenye maambukizi.

“Idara ya afya tumejitahidi kuweka tahadhari katika maeneo yote ya mipakani ikiwemo katika maeneo ya bandari zote, kiwanja cha ndege na maeneo ambayo yanaingilika kwa urahisi na jamii kuingia na kutoka, pia tumeweka tahadhari kwa kuwa na wataalamu pamoja na vifaa vya kufanyia vipimo lengo ni kuhakikisha mkoa unakuwa salama” amesema

Mambukizi ya Ugonjwa wa Ebola hadi sasa umeripotiwa nchini Uganda mwezi Septemba mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments