WANNE WASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA UNYANG'ANYI NA UJANGILI KIGOMA

 

Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma Kamishna Msaidizi wa Polisi Filemon Makungu akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake hii leo. (Picha na Isaac Aron Isaac)

Baadhi ya mashine za boti zilizokutwa kwa watuhumiwa wa matukio ya unyang'anyi. (Picha na Isaac Aron Isaac) 

Na Isaac Aron Isaac, Kigoma

JESHI la Polisi Mkoani Kigoma linamshikilia Yamungu Dunia mkazi wa Kibirizi manispaa ya Kigoma Ujiji kwa tuhuma za unyan'ganyi wa zana za uvuvi za boti aina ya Yamaha zenye thamani ya shilingi milioni 46 akiwa amezihifadhi katika ghara bila uhalali wa umiliki.

Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma Kamishna Msaidizi wa Polisi Filemon Makungu amesema tukio hilo la unyang'anyi liliripotiwa mkoani Rukwa na hivyo kuamua kufanya oparesheni ya pamoja na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mnamo Oktoba 20, 2022.

Jeshi la polisi limemsafirisha mtuhumiwa pamoja na kielelezo kwenda mkoani Rukwa kwaajili ya hatua zaidi za kisheria

Katika hatua nyingine jeshi la polisi kwa kushirikiana na askari wa hifadhi ya Gombe limewakamata Bahati Sondese, Hisea Samweli na Yared Daniel wote wakulima kutoka wilaya ya Kasulu kwa kupatikana na nyara za serikali ikiwemo vipande viwili vya pembe za ndovu vyenye uzito wa kilogram nane vyenye thamani ya milioni 34 kinyume na sheria

Watuhumiwa walikamatwa wakiwa wamehifadhi nyara hizo ndani ya begi wakiwa wanatafuta mteja wa kumuuzia katika eneo la Murubona tarafa ya Heru chini na kwamba watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Jeshi la polisi mkoani Kigoma limetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa za kihalifu ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa zaidi.

 

 

 

Post a Comment

0 Comments