AKINA MAMA WATAKIWA KUNYONYESHA WATOTO WAO KWA MUDA WA MIEZI SITA MFULULIZO

 


Na Mwajabu Hoza , Kigoma 

MKUU wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye ametoa wito kwa wakinamama kuhakikisha wananyonyesha watoto wao kwa kipindi chote cha miezi sita mfululizo bila kuwapa chakula chochote hadi hapo watakapotimiza miezi sita.

Akizungumza na wananchi wa kijiji Mlela kata ya Kandaga wilaya Uvinza amesema asilimia kubwa ya akinamama ambao wamejifungua wamekuwa hawafuati maelezo ya wataalamu ya kuwanyonyesha watoto miezi sita mfululozo kwani wamekuwa wakiwapa na chakula jambo ambalo ni kinyume na maelekezo ya wataalamu wa afya .

Andengenye amesema mtoto anapaswa kunyonya miezi sita mfululizo na baada ya kutimiza  miezi sita ndipo mtoto atatakiwa kuanza kunywa uji wenye virutubisho muhimu ambavyo wataalamu wamekuwa wakitoa elimu kuwapatia watoto mara baada ya kutimiza miezi sita.



Amesema ukiachilia mbali kuwapa chakula watoto wakiwa wametimiza miezi sita lakini pia ni muhimu kuendelea kuwanyonyesha hadi hapo watakapotimiza miaka miwili, jambo ambalo linasaidia kumjenga mtoto kiafya, kimwili na kiakili kwa kuwa maziwa ya mama yanavirutubisho vingi kwa afya ya mtoto.

Sambamba na hilo amesema mkoa wa Kigoma unazalisha vyakula vingi vya aina mbalimbali lakini imekuwa ngumu familia kuandaa mlo kamili ambao ni lishe bora na waadhirika wakubwa ni watoto ambao hukumbwa na tatizo la utapiamlo kutokana na kutozingatia makundi muhimu matano ya vyakula.

Baadhi ya wananchi akiwemo Josephina Edwer amesema suala la akinamama kuacha kunyonyesha watoto wao linasababishwa na uelewa mdogo wa namna gani watoto wanapata virutubisho bora kupitia maziwa ya mama hivyo ni lazima elimu itolewe kwa wingi ili watambue umuhimu wa kimnyonyesha mtoto kwa miezi sita mfululizo lakini pia kwa kipindi cha miaka miwili.

Sambamba ni hilo baadhi yao wanahofia kuharibu maziwa yao kwa kunyonyesha watoto wao na hivyo wengi huacha kunyonyesha watoto kwa kipindi cha miaka miwili na hata kama wakiwanyonyesha hawawapi maziwa ya kuwatosheleza hadi wakashiba.

Anastazia Amos  amesema changamoto nyingine ni ukosefu wa elimu ya jinsi ya kuandaa mlo kamili hususani kwa watoto kulingana na umri wao na ni chakula cha aina gani wanapaswa kupatiwa hivyo mara kadhaa maeneo ya vijijini wanawapa watoto wadogo chakula chochote kilichopo bila kujali mpangilio wa lishe bora.

“Asubuhi unakuta mtoto anapewa ugali tena umepowa na maharage na mchana anakula tena hivyo hivyo na mara nyingi familia inachojali  ni mtoto kushiba na sio amekula chakula cha aina gani” alisema .

Hezra Boniphasi  yeye anasema wakati wa masika familia nyingi zinahamia mashambani na chakula kikuu ni ugali, mihogo na viazi hapo hakuna mbogamboga wala matunda na hicho chakula anapewa hata yule mtoto ambaye hajatimiza  miaka miwili hivyo inakuwa vigumu kwa watoto wa aina hii kuwa na afya bora kulingana na lishe inayoelekezwa.

Muuguzi mkuu wilaya ya Uvinza Festo Bujiku anasema endapo mtoto hatukuwa na lishe bora akiwa tangu yupo tumboni hiyo inamuadhiri katika ukuaji wake na ndio maana kwa sasa serikali ya awamu ya sita imeamua kuwekeza zaidi katika mpango mkakati wa lishe kwa jamii ikiwemo kutoa elimu namna ya kuandaa chakula na jinsi bora ya mama kumnyonyesha mwanae.

Bujiku anaeleza dalili za mtoto ambaye ameadhiriwa na lishe isiyo bora ambayo inachangia utapiamlo kuwa ni pamoja na mtoto kupungua uzito ambao haulingani na umri wake , urefu, kukunjamana kwa ngozi, kuvimba mwili na mwili kudhohofu na ili kuondokana na hilo ni lazima jamii ihakikishe mlo wa mtoto unakuwa na aina tano ya vyakula.   


  

Post a Comment

0 Comments