UJENZI WA CHUJIO LA MAJI SULUHISHO LA MAJI SAFI KIBONDO

 

Chujio la maji la chanzo cha Mgoboka kinachosambaza maji kwa wananchi wa Kibondo mjini.

Chujio la maji la chanzo cha Mgoboka kinachosambaza maji kwa wananchi wa Kibondo mjini

Na Fadhili Abdallah, Kigoma

UJENZI wa chujio la maji katika chanjo cha maji cha Mgoboka kinachotoa huduma kwa wakazi wa mji wa Kibondo inaelezwa kuwa umewezesha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi hao wakiondokana na adha ya kupata maji yaliyojaa tope.

Meneja wa Wakala wa maji mjini na vijijini (RUWASA),Mohamed Almas akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma alisema kuwa kwa mwaka uliopita wilaya ilipokea kiasi cha shilingi Bilioni 2.4 kwa ajili ya miradi mitano ikiwa ni fedha za serikali na wadau wa maendeleo walitoa bilioni 4.1 kwa miradi mine  na mradi mmoja wa kutafuta vyanzo ambao haujaanza.

Almasi alisema kuwa miongoni mwa miradi ambayo waliisimamia na kuwa ni kipaumbele kuhakikisha inakamilika ni pamoja na ujenzi wa chujio la kuchuja maji katika chanzo cha Mgoboka ambacho kilikuwa na malalamiko makubwa kutoka na maji yanayosambazwa hasa wakati wa mvua kuwa tope tupu.

“Kwa sasa chujio limejengwa ambalo licha ya kufanya maji yanayosambazwa kuwa safi lakini pia maji hayo kwa sasa ni salama kwani dawa inayowekwa inawezesha kuua wadudu hivyo watu wanaotumia maji hayo moja kwa moja hawapo kwenye athari ya kupata magonjwa ikiwemo magonjwa ya tumbo,”Alisema Meneja huyo wa RUWASA wilaya Kibondo.

Alisema kuwa baada ya kutekelezwa kwa miradi hiyo  10 ambayo kati yake miradi sita imekamilika wilaya ya Kibondo imeongeza huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi na kufikia asilimi 69.

Akizungumzia ujenzi wa chujio hilo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya Kibondo, Dk.Chitupilla Gabriel alisema kuwa ujenzi wa chujio katika chanzo cha maji cha Twabagondozi ni muhimu kwao kwa matumizi ya kawaida na maendeleo kwa wakazi wa mji huo.

Chitupila alisema kuwa maji hayo yanatumika pia kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo hospitali hivyo kuwepo kwa maji ambayo yanatope yalilazimu kutumia fedha nyingi kutibu maji wanayotaka kutumia lakini pia imekuwa na athari kwa jamii katika suala zima la magonjwa ya tumbo ambapo kwa sasa hali ni tofauti.

Baadhi ya wananchi wa mji wa Kibondo akiwemo Ayubu Gabriel mkazi wa Kata ya Kibondo mjini alisema kuwa kwa sasa wanatumia maji safi na salama na kuondokana na kutumia maji ya tope ambayo yalifanya watu watafute maji kwenye visima.

 

Post a Comment

0 Comments