UJENZI WA STEND KUONGEZA MAPATO YA HALMASHAURI KAKONKO

 

Jengo la Standi ya Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma ambalo ujenzi wake unaendelea

Jengo la Standi ya Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma ambalo ujenzi wake unaendelea


Na Fadhili Abdallah, Kigoma

Ujenzi wa stendi mpya ya mabasi na ya kisasa katika wilaya ya Kakonko imeelezwa kuwa utaongeza mapato ya ndani ya halmashauri ya wilaya Kakonko kwa kiasi kikubwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya Kakonko,Michael Faraay akizungumza ofisini kwake wilayani humo alisema kuwa halmashauri hiyo  imekuwa moja ya halmashauri zenye vyanzo vichache vya mapato ya ndani hivyo mradi huo utaongoza mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.

"Mwaka jana tuliongeza mapato ya ndani kufikia bilioni moja kutoka milioni 600 na mradi huu utawezesha mpango wa halmashauri  kuongeza mapato ya ndani kufikia bilioni 2," alisema Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Kakonko.

Akitoa maelezo kwa waandishi wa habari eneo la mradi Mhandisi ujenzi wa halmashauri ya wilaya Kakonko, Kiza Mkoko alisema kuwa miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kuwezesha kuongeza mapato katika stendi hiyo ni pamoja na vibanda 27  vya maduka ambavyo vitakodishwa, maeneo kwa ajili ya ukodishaji huduma za kibenki, vibanda vya kukatia tiketi, Mgahawa wa vyakula na vinywaji na magari yatakayokuwa yanaingia ndani ya stendi hiyo.

Mkoko alisema kuwa mradi huo ambao ulianza mwaka 2019 uko kwenye hatua za ukamilishaji baada ya kusimamama kwa mwaka mzima mwaka jana na unatarajia kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 2.

Mkuu wa wilaya Kakonko,Kanali Evance Malasa akizungumzia mradi huo alisema kuwa kwao huo ni moja ya miradi ya kimkakati katika kuinua mapato ya halmashauri na kwa sasa uko kwenye hatua nzuri za ukamilishaji.

Malasa alisema kuwa pamoja na lengo kuu la kuongeza mapato ya halmashauri lakini alisema kuwa unalenga kuboresha huduma kwa wananchi ambao wanatumia stendi hiyo kutokana na kuwepo kwa huduma mbalimbali lakini stendi hiyo ni moja ya stendi za mfano kwa mkoa Kigoma.

Baadhi ya wananchi wa wilaya Kakonko akiwemo Justin Malinusi alisema kuwa kuwepo kwa stendi hiyo kutawasaidia wananchi kwani watakuwa wamepata mahali pazuri na bora kwa ajili ya kusubiri usafiri wa kwenda maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya mkoa.

 

 

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Michael Faraay akizungumza na blog hii ofisini kwake kuhusu ujenzi unaoendelea wa standi ya wilaya hiyo.

Post a Comment

0 Comments