WILAYA YA KIBONDO KUKABILIANA TATIZO LA UTAPIAMLO

 

Mkuu wa idara ya Afya , lishe na ustawi wa jamii wilaya ya Kibondo
Dkt. Henry Chinyuka akizungumza na waandishi wa habari kuhusu suala la lishe. 

Na Mwajabu Hoza, Kigoma

Halmashauri ya wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma imeeleza kujipanga kutekeleza mpango  mkakati wa kukabiliana na afua za lishe katika wilaya hiyo kwa kutenga bajeti ili kuondokana na tatizo la utapiamlo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Akizungumzia hilo Mkuu wa idara ya Afya,lishe na ustawi wa jamii wilaya ya Kibondo Dkt. Henry Chinyuka amesema hali ya utapiamlo kwa watoto kwenye halmashauri ya wilaya  hiyo ni asilimia 32.

Dkt. Chinyuka amesema kwa kipindi cha serikali ya awamu ya sita kwa mwaka 2021 msisitizo mkubwa ulielekezwa  kwenye utoaji wa fedha ambapo halmashauri ilitoa zaidi ya asilimia 80 ya fedha zote zilizotengwa ambazo zilitumika katika utekelezaji wa afua za lishe ngazi ya jamii.

Amesema kwa mwaka 2022 halmashauri imetenga milioni 62 ambapo hadi sasa imetoa milioni 29 na kufikia June 2023 halmashauri itakuwa imetoa fedha zote ambazo zimetengwa kwa lengo la utekelezaji wa afua za lishe.

“ Fedha hizo zitatumika katika makundi mawili moja ni kupata chakula na dawa, hii ni kwa ajili ya watoto wenye utapiamlo mkali ambayo itawasaidia kurudisha kinga zao na kurutubisha miili yao, na fedha zingine zinatumika kwa ajili ya kutoa elimu ya jiko darasa namna ya kupika chakula bora kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano” amesema Chinyuka. 

Baadhi ya akinamama akiwemo Salma Hashim anaeleza elimu ambayo wanapatiwa kutoka kwa wataalamu imekuwa ikisaidia kuboresha afya za watoto lakini changamoto kubwa ni ushirikiano wa wanaume kwenye utekelezaji wa elimu hiyo.

Salma anaeleza namna bora ya  kuandaa lishe  kwa mtoto kama ambavyo wameelekezwa kuwa ni pamoja na kuwapa watoto matunda kabla ya kuwapatia uji wa asubuhi, lakini pia kuandaa uji ambao utakuwa na lishe bora kwa kuchanganya unga wa sembe, mchicha pamoja na Karanga.

“ Mafunzo ya jiko darasa yamekuwa na msaada mkubwa katika kuboresha afya za watoto lakini  wanaume wamekuwa kikwazo pale inapohitajika kuchangia chakula ambacho tunapaswa kuandaa kwa ajili ya watoto, wanaume hawatoi ushirikiano lakini pia mazoea ya kuandaa chakula cha aina moja nyumbani nalo hilo ni tatizo.” Alisema

Christian Kilonza amesema licha ya kuzalisha vyakula vya aina mbalimbali haswa maeneo ya vijijini bado watoto wanakuwa na tatizo la utapiamlo na hilo linatokana na wazazi kutokuwa na muda wa kuhudumia watoto wao kutokana na kujishughulisha na shughuli za shamba na kuwaacha watoto wakilelewa na watoto wenzao na hivyo inakuwa ngumu kuwapatia chakula kwa wakati. 

Katika kukabiliana na hali hiyo serikali inaendelea kutilia mkazo suala la elimu kuendelea kutolewa kwa jamii ili kuona umuhimu wa kuwapatia watoto wao lishe bora wakati wote na  kuwaepusha na  hali ya utapiamlo.

Hivi karibuni ofisi ya mkuu wa mkoa Kigoma iliingia mkataba na wakuu wa wilaya zote za mkoa wa Kigoma pamoja na wakurugenzi wote namna bora ya utekelezaji wa afua za lishe kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa mkoa wa Kigoma. 

Lakini pia katika utekelezaji wa program Jumuishi ya Taifa ya malezi, Makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT – MMMAM)  wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto kupitia Taasisi ya chakula na lishe Tanzania inaandaa mwongozo wa Kitaifa wa utoaji wa chakula na lishe kwa wanafuzi wa elimu ya msingi.

 

 

Post a Comment

0 Comments