ACT WAZALENDO YAWATAKA WAZEE KUIPIGIA KELELE SERIKALI KUHUSU MATIBABU



Na Fadhili Abdallah, Kigoma.

Chama  Cha ACT Wazalendo kimewataka viongozi wa ngome ya wazee ya chama hicho kutumia nafasi kuipigia kelele serikali kutekeleza mipango ambayo italeta unafuu wa maisha kwa watanzania ikiwemo upatikanaji wa matibabu bure.

Katibu Mkuu wa ACT Ado Shaibu alisema hayo wakati akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa nembo ya ngome ya wazee ya Chama hicho uzinduzi uliofanyika mjini Kigoma na kusema kuwa wazee ni tunu ya Taifa na kwamba serikali inapaswa kuwa enzi kwa namna ya pekee badala ya kuwaacha kuhangaika kama walivyo sasa.

Akizungumzia uzinduzi wa nembo ya ngome ya wazee Shaibu alisema kuwa huo ni mwanzo mpya kwa wazee hao kuona wanabeba jukumu la kusimamia utekelezaji wa mambo mbalimbali yenye faida kwa wazee wote wa Kitanzania na siyo kuishia kuzindua nembo kama alama ya Jumuia hiyo ya wazee lakini iwe kwa niaba ya watanzania.

Alisema kuwa lazima wazee wa chama cha ACT – Wazalendo kusimama kwa niaba ya wazee wa Tanzania kupigania masuala ya msingi yanayowahusu ikiwemo suala la matibabu bure kwa wazee, upatikanaji wa mikopo na ruzuku kwa ajili ya miradi ya kiuchumi kutoka halmashauri kama ilivyo kwa makundi ya wazee na vijana.

Katika hatua nyingine Katibu huyo wa ACT Wazalendo alisema kuwa kamati kuu ya chama hicho inatarajia kukutana hivi karibuni kupitia ripoti na mapendekezo ya kikosi kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa nchini na baada ya hapo watatoa msimamo wa chama kuhusu ripoti hiyo na mapendekezo yaliyotolewa.

kiongozi huyo alisema kuwa watatoa msimamo wa mambo wanayokubaliana nayo na wasiyokubaliana nayo na hata wanayokubaliana nayo watataka serikali iwe na muda wa utekelezaji wa mapendekezo hayo na kuonyesha dhamira ya ukweli ya kukubali ripoti hiyo.

Awali akisoma risala kwenye uzinduzi huo Katibu Mwenezi Taifa na mahusiano ya Umma ACT – Wazalendo, Ally Omari alisema kuwa uzinduzi wa nembo ya wazee ni kutaka kutumia nafasi yao kama wazee kupigania haki na mahitaji mbalimbali ya kibinadamu kwa wazee ambayo utekelezaji wake haufanyiki.

Omari alisema kuwa serikali chini ya Chama Cha Mapinduzi inaeleza mambo mengi kuhusu masuala ya wazee lakini utekelezaji wake haufanyiki na mipango hiyo imeishia kwenye karatasi hivyo wazee wa ACT wazalendo wanataka kusimamia jambo hilo kuona serikali inasimamia kwa vitendo mambo yanayoahidiwa na kutekelezwa na wazee.

Mwenyekiti wa Ngome ya Wazee Taifa, Yassin Mohamed akizungumza katika mkutano huo alisema kuwa bado utekelezaji wa masuala mengi kwa wazee hayafanyiki na haya yameshuhudiwa maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye upatikanaji wa huduma za matibabu.

Post a Comment

0 Comments