TARI KIBAHA YAPONGEZWA KWA KUSAMBAZA MBEGU BORA ZA MIWA KWA WAKULIMA



Na Mwandishi Wetu, Kilombelo

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero mheshimiwa Hanji Godigodi ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo kituo cha Kibaha kwa kuzalisha mbegu bora za miwa na kuzisambaza kwa wakulima.

Mheshimiwa Godigodi ametoa pongezi hizo katika hafla ya usambazaji wa mbegu bora za miwa kwa wakulima iliyofanyika katika kijiji cha Msolwa Ujamaa Wilayani Kilombero.

Mheshimiwa Godigodi amesema kwamba maamuzi ya TARI Kibaha ya kuzalisha mbegu bora kwa wakulima baada ya kufanya utafiti ni hatua kubwa katika kuboresha Kilimo nchini.



"Kwa kweli nimefurahishwa sana na tukio hili kwasababu nimeshuhudia mashamba ya mbegu yakiwa na ubora wa hali ya juu,huku ni kutekeleza kwa vitendo maagizo ya mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan",amesema mheshimiwa Godigodi.

Mheshimiwa Godigodi amewataka watafiti wa TARI kibaha kuendelea na zoezi la uzalishaji wa mbegu bora za miwa wilayani Kilombero ili kukidhi mahitaji ya kiwanda cha sukari.

Meneja wa TARI Kibaha Dkt Nessie Luambano amesema TARI Kibaha imedhamiria kufanya mapinduzi makubwa ktk uzalishaji wa mbegu bora za miwa nchini kwa kuongeza mashamba na Utafiti wa mbegu.

Kwa upande wake mratibu wa zao la miwa nchini Bi.Minza Masunga amesema mbegu hizo bora zilizozalishwa katika kijiji cha Msolwa Ujamaa ni kutekeleza kwa vitendo maagizo ya serikali ya kutaka wakulima kupatiwa mbegu bora ili waweze kupata tija.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TARI bi.Margareth Mchomvu amesema mambo yanayofanywa na TARI Kibaha ni miongoni mwa kazi nyingi zinazofanywa na Taasisi hiyo katika vituo vyake vyote 17.



 

Post a Comment

0 Comments