Na Emmanuel
Matinde, Kasulu Kigoma
Wananchi wa Kaya takribani 400 katika Vijiji vya Kumtundu
na Mvugwe katika Kata ya Nyamidaho Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani
Kigoma, wamelalamikia hatua ya serikali wilayani humo ya kuwaondoa katika
maeneo waliyokuwa wakiishi na kufanya shughuli za kilimo na kupewa mwekezaji wa
shamba la miwa na kiwanda cha sukari bila kuwalipa fidia yoyote.
Wakitoa malalamiko yao wananchi hao walisema mbali na
kuondolewa pia mazao yao waliyokuwa wamelima yametaifishwa na nyumba zao
kubomolewa ambapo wamesema wao hawapingi mwekezaji kuwekeza katika maeneo hayo,
lakini hatua ya serikali kuwafurusha bila kuwalipa fidia ni kinyume na
makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa kuridhia maeneo yao yatumike kwa
ajili ya uwekezaji.
Aidha katika upande mwingine wa mgogoro huo wananchi hao
waliishutumu serikali ya wilaya ya Kasulu kwa kuchochea mgogoro baina ya
wananchi baada ya kukata sehemu ya ardhi inayomilikiwa kihalali na baadhi ya
wananchi wa kitongoji cha Mnarani eneo la Mkuyuni na kuwagawia wale
walioondolewa katika eneo la uwekezaji.
Akizungumzia eneo linalolalamikiwa na wananchi hao lenye
ukubwa wa hekta takribani elfu 38 Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isaac
Mwakisu, alisema eneo hilo linamilikiwa kisheria na Kituo cha Uwekezaji
Tanzania TIC ambalo walilipata kutoka kwa wananchi mnamo mwaka 2009.
0 Comments