DHAMIRA YA SERIKALI NI KUPAMBANA NA MAGONJWA YASIYOYAKUAMBUKIZA

Na Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amesema dhamira ya Serikali ni kupambana na magonjwa yasiyoambukiza hivyo Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ina mchango mkubwa katika kutibu na kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza hivyo usimamizi wa Hospitali ya Dar Group chini ya JKCI kutasogeza karibu huduma za matibabu ya kibingwa ya moyo kwa wananchini.

Prof Nagu amesema hayo leo kwenye ziara ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu aliyoifanya katika Hospitali ya JKCI Dar Group kuona hali ya utoaji huduma za afya.

Prof. Nagu amesema pamoja na kupanua wigo wa huduma, Serikali itaendelea kuhimiza ubora wa huduma zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

“Tuangalie ubora wa huduma kwa kuangalia mahitaji ya mteja, mteja anataka huduma salama, bora na inayopatikana kila wakati kwa haraka na haya ndio mambo ambayo tunasisitiza kila siku” amefafanua Prof. Nagu.

Hata hivyo ameipongeza Taasisi ya JKCI kwa kuipokea Hospitali ya Dar Group kwa vitendo na kuanza maboresho ya huduma kwa haraka katika kipindi cha miezi miwili.

Hapo awali Hospitali ya Dar Group ilijengwa kwa ajili ya kutoa Huduma za Afya kwa wafanyakazi wa Viwandani na kusimamiwa na Msajili wa Hazina. 

Mnamo mwezi Novemba 2022 Serikali kupitia Wizara ya Fedha, Msajili wa Hazina walifanya maamuzi ya kuichukua Hospitali hiyo na kuipatia Wizara ya Afya kwa ajili ya usimamizi na kutatua changamoto za kiutendaji zilizokuwepo hapo awali.

Post a Comment

0 Comments