ELIMU YA MICHEZO KULETA MATOKEO CHANYA YA UJIFUNZAJI SHULE ZA MSINGI

 


Na Mwajabu Hoza, Kigoma

SHULE za msingi zilizopo maeneo yanayozunguka kambi za wakimbizi katika wilaya ya Kibondo na Kasulu mkoani Kigoma, zimeanza kunufaika na elimu ya ujifunzaji kupitia mbinu za kimichezo na walengwa wakiwa ni wanafunzi wenye umri kuanzia miaka mitatu na lengo ni kuwafanya wanafunzi hao kuipenda shule pamoja na kuwakinga na vitendo vya ukatili katika jamii.

Kaim afisa elimu msingi Mwalimu Josefu Maiga kutoka wilaya ya Kasulu amesema ufundishaji wa kutumia michezo kwa shule za msingi hususani kwa wanafunzi wa awali na darasa la kwanza inawajenga  kuipenda shule hivyo walimu wanawajibu mkubwa wa kuwa wabunifu katika michezo hiyo ambayo itakuwa na tija kwao na  kuona shule ni sehemu ya kujifunza na sio sehemu ya adhabu.

Amesema michezo mara nyingi inasaidia kuamsha hari ya kujifunza, kuleta ubunifu, inahamasisha watoto kupenda kudadisi na kujifunza, pia kumjenga mwanafunzi kijamii kwa kudumisha mshikamano, undugu na urafiki.

Maiga amesema kwa sasa halmashauri ya wilaya ya Kasulu inatekeleza ufundishaji wa aina hiyo katika shule tano ikiwa kama hatua za awali za majaribio ambapo hadi sasa  shule ya msingi Mvugwe Nyamidaho, Mkambati, Nyamganza na shule ya msingi Kumtundu ndio zimefikiwa na elimu hiyo. 

Amesema elimu hiyo kupitia michezo inatakiwa kuwa chachu ya kuongeza idadi ya wanafunzi shuleni hasa kwa wale  ambao wanaanza elimu ya awali ikiwa elimu hiyo kwao  ndio msingi wa kuwajenga kiakili na ukuaji wa ubongo. 

Ufundishaji wa aina hiyo pia unachangia kuondoa utoro, mimba na  vitendo vya ukatili kwa watoto ambapo afisa maendeleo ya jamii wilaya ya Kasulu Subira Swai anasema michezo hiyo inachangia watoto kuwa pamoja na kuzoeana na hivyo kuondoa vitendo vya ukatili kwa watoto.

“Hii michezo hujenga urafiki na umoja , na kurahisisha wanafunzi kumshirikisha mwenzake vitendo vya ukatili ambavyo wanapitia katika maeneo yao wanayoishi lakini pia inawafanya watoto kuchoka na hivyo kurudi nyumbani na kupata muda wa kupumzika na kuacha kwenda kwenye kumbi za video pamoja na kushiriki kufanya biashara ndogondogo” alisema 

Mwalimu Yusuph Ibrahimu kutoka shule ya Msingi Kisuma anasema ufundishaji kwa njia ya michezo umesaidia sana katika shule hiyo kupunguza utoro wa wanafunzi licha ya kukutana na  changamoto ya  mapokea ya jamii, wazazi na walezi kuona kuwa ujifunzaji wa aina hiyo unachangia wanafunzi kutosoma vizuri na wengine kudai kuwa unahamasisha matukio maovu kwa watoto.

Ibrahim amesema ukiachilia mbali jamii lakini pia bado kuna baadhi ya walimu bado hawajawa na uelewa wa kutosha kufundisha wanafunzi kupitia michezo hivyo bado elimu inahitajika kwa walimu ili waweze kuendelea kutoa elimu bora yenye kumfanya mwanafunzi aelewe kwa vitendo.

" Tumekuwa tukifundisha kupitia zana mbalimbali za michezo ambazo walimu na wanafunzi huzitengeneza , nyimbo , na maigizo na lengo ni kuwajengea uelewa wanafunzi kwa vitendo hususani wale wanafunzi wanaosoma chekechea hadi darasa la nne wanakuwa na tabia ya kuipenda sana shule na hapo ndio msingi wa kumjenga mtoto kiakili akiwa na umri wa miaka minne na kuendelea. 

Scollastica Alexandra na Josephina Joseph ni baadhi ya wazazi ambao wanaeleza ufundishaji wa kutumia michezo umekuwa na manufaa zaidi na hivyo kuomba michezo hiyo kufundishwa zaidi darasa la awali na darasa la kwanza ambao wanapenda sana michezo lakini pia wazazi nao wapatiwe elimu hiyo ili kipindi cha likizo waweze kushiriki na watoto wao majumbani.

Wamesema serikali na wadau wamebuni mbinu nzuri ambayo itawajenga watoto kuwa na uimara wa kimwili na kiakili lakini pia itasaidia kupunguza tabia ya wazazi kuwatumikisha watoto wao kwenye shughuli za uzalishaji mali kwani wameona umuhimu wa michezo kwa watoto wao.

Mshauri wa elimu ya awali wa malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto kutoka  Shirika la Children Incrossfire (CIC) Davis Gisuka amesema mbinu za kimichezo zinasaidia watoto katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuwajenga katika stadi za ubunifu, kutatua matatizo , ushirikiano , kuwasiliana, kuwa wagunduzi, wadadisi  pamoja na kuchangamana na stadi nyingine za maisha.

Lakini pia amesema michezo inawakuza watoto kimwili, kiakili, kihisia na kijamii na hivyo kumfanya mtoto akuwe kwa utimilifu wake. 

Amesema kupitia michezo hiyo watoto wanagundua mazingira yanayowazunguka na kujifunza taarifa mbalimbali ambazo ni mpya ambapo katika kipindi cha miaka ya awali pale wanapozaliwa  ubongo unaunda miunganiko mingi kuliko hata matarajio ya ubongo wenyewe.

"Miunganiko hiyo ambayo inatumika mara kwa mara inaendelea kuimarishwa na kutengeneza mtandao wa miunganiko imara zaidi kwa mtoto na ile ambayo haitumiki mara kwa mara huondolewa kwa njia inayoitwa prunning" amesema.

Hivyo michezo ni muhimu sana katika makuzi ya ubongo wa mtoto kwa sababu inatoa fursa kwa watoto kupata uzoefu mpya na kukuza stadi alizo nazo ambazo zinaimarisha mtandao wa miunganiko ndani ya ubongo nani mara tu baada ya kuzaliwa hadi  anapofikisha umri wa miaka nane.

Ukiachilia mbali miunganiko hiyo lakini pia wakati wa michezo mtoto hujenga stadi za mawasiliano, uchangamani, huruma, kusaidiana, upendo urafiki na undugu pamoja na kutambua mambo mengi ikiwemo ujasiri , kujiamini na umahiri.

Mpango Jumuishi wa Taifa wa Malezi ,Makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT-MMMAM) ya 2021/22  hadi 2025/26 kwa watoto wenye umri wa miaka 0-8 kwenye jedwali la  matokeo ya muda mfupi inaeleza fursa za ujifunzaji wa awali zimeongezeka kutoka bilioni 605.20 kwa mwaka 2021/22 na kufikia bilioni 145. 14 kwa mwaka 2025/ 2026 katika kuhakikisha mpango huo unatekelezeka na kuleta matokeo chanya. 

Mwaka 2022 shirika la kuhudumia wakimbizi IRC lilianza kutekeleza mradi wa PLAYMATTERS ambao utekelezwa wilaya ya Kibondo na Kasulu ambapo shule tano za wilaya ya kasulu zimefikiwa na lengo ni kufundisha kupitia michezo ili kuleta uelewa kwa wanafunzi  namna ya ufundishaji na kujifunza kupita michezo.

Sofia Kosmasi kaimu Meneja Mradi wa PLAYMATTERS kutoka IRC amesema mara baada ya kuanza kwa mradi huo kumekuwa na matokeo chanya ambapo awali utekelezaji ulikuwa katika shule moja lakini kutokana na mabadiliko makubwa ya kujifunza kupitia michezo imelezimika kuongeza shule zingine na kufikia tano.

Amesema IRC kushirikiana na serikali wataendelea kuona maendeleo ya mradi huo ili kuweza kuongeza wigo hususani katika kuwapatia elimu hiyo walimu wa shule mbalimbali ili nao waweze kufundisha wanafunzi kwa ufasaha zaidi.

 

Post a Comment

0 Comments