MAJALIWA: TULINDE MBOLEA YA RUZUKU ILIYOTOLEWA NA RAIS DKT. SAMIA

Na Mwandishi Wetu, Mbeya
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi kuwa walinzi wa mbolea ya ruzuku iliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ya kuongeza uzalishaji wa mazao katika msimu wa 2022/2023.

Amesema kuwa kumekuwa na watanzania wachache wasiokuwa na nia njema wanaotorosha mbolea kwenda nchi jirani na kuwaacha watanzania bila kuwa na mbolea ya kutosha ”jambo hili lazima tulikemee na tulisimamie sote ili kuhakikisha mbolea iliyopo nchini ni kwa ajili ya watanzania, kila mmoja awe mlinzi kwa mwenzake”

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Januari 16, 2023) wakati akisalimia na wananchi kwenye eneo la Mbalizi jijini Mbeya akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali. Amesema utoaji wa ruzuku hiyo ya mbolea unalenga kuongeza uzalishaji wa chakula nchini na ni marufuku kuiuza nje.

Ameongeza kuwa awali mbolea iliuzwa kwa zaidi ya shilingi 100,000 lakini Mheshimiwa Rais Dkt. Samia akaridhia kutoa ruzuku shilingi bilioni 150 ili ikashushe bei ya mbolea na sasa inauzwa kwa shilingi 70,000. ”Tusikubali fedha hiyo kutumika nje la malengo, tulinde mbolea yetu isiuzwe kwa wasiohusika.”

”Nimefurahi sana kwa hatua zilizochukuliwa mkoani Songwe, tani 2199 zimekamatwa zikipelekwa nchi jirani hii haikubaliki, watanzania tuwe walinzi hii ni pesa yetu inatoroshwa na wachache, malengo yetu ni kuwahudumia ninyi kwa usimamizi wa Rais Dkt. Samia”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuelekeza hatua zilizofikiwa katika maendeleo ya uboreshwaji wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Songwe kuwa tayari njia ya kurukia ndege imekamilika kwa asilimia 100, jengo la abiria ujenzi umefikia asilimia 96 na sasa zoezi la ufungaji taa linaendelea na litakapokamilika uwanja huo utatumika wakati wote.

”Tunafanya hivi ili kuvuta masoko kutoka nchi jirani ikiwemo Kongo, Zambia na malawi walete ndege zako, haya yote yanafanywa na Rais wetu Dkt. Samia kwasababu ana maono ya mbali na dhamira yake ya dhati ya kuwaletea watanzania maendeleo.”

Post a Comment

0 Comments