NAIBU WAZIRI ENG. KASEKENYA ARIDHISHWA NA MAANDALIZI YA UJENZI WA BRT III


Na Muhingo Mwemezi, Dar Es Salaam

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya ametembelea Ujenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka BRT na kueleza kuridhishwa kwake na maandalizi ya kuanza kwa ujenzi wa awamu ya tatu ya mradi huo kutokea Katikati ya Jiji la Dar es Salaam kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere hadi Gongolamboto KM 24.3.

 

Naibu Waziri Kasekenya katika ziara hiyo amekagua atua ya awali ya Mkandarasi wa Kampuni ya Sinohydro aliyeanza kukusanya vifaa na mitambo ya kuanza kazi ya ujenzi wa Awamu ya Tatu ya BRT.

 

Amesema mitambo aliyoiona eneo la mradi inaonesha namna Mkandarasi Sinohydro alivyojipanga kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.

 

"...Mkandarasi huyu ndiye anayejenga pia awamu ya pili ya BRT, kwa maana ya uandaaji wa vifaa kwenye eneo la mradi inaridhisha kabisa na maandalizi haya, "...Kwa maana ya kujiandaa kwa kweli amejipanga, nimeongea pia na Mhandisi Mshauri kwenye mikataba kuna vitu ambavyo Mkandarasi inabidi avilete na tayari amevileta hivyo tuna hakika atafanya kazi nzuri," alisema Naibu Waziri Kasekenya.

 

Aidha ameagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha wanafanya uchunguzi ili kujiridhisha na wataalam walioletwa kutekeleza mradi huo kama ndivyo walioainishwa kwenye makubaliano ya mkataba huo.  


Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha changamoto zote za foleni na msongamano katika usafiri kwa jiji la Dar es Saalam inamalizika mara baada ya kukamilika kwa miradi hiyo.


Akizungumza mara baada ya maelekezo ya Naibu Waziri, Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam, Eng. Harun Senkuku  amesema wamepokea maelekezo ya Mhe. Naibu Waziri na kuahidi kuyafanyia kazi kama ilivyoelekezwa.

 

Post a Comment

0 Comments