RAIS SAMIA AWAHAKIKISHIA USHIRIKIANO MABALOZI WA NCHI ZA NJE NA MASHIRIKA YA KIMATAIFA

Na Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewahakikishia Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao hapa nchini.

Mhe. Rais Dkt. Samia alitoa ahadi hiyo tarehe 13 Januari, 2023 katika Sherehe za Mwaka Mpya 2023 kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, katika sherehe hizo Mhe. Dkt. Samia alisema licha ya changamoto za uviko 19 zilizoikumba Dunia kwa ujmla, uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa himilivu. “mfano kwa mwaka 2022 pato la taifa limekua kwa asilimia 4.7 ukilinganisha na asilimia 4.3 mwaka 2021, na kwa mwaka 2023 tunategemewa utaongezeka na kufikia asilimia 5,” alisema Dkt. Samia

Rais pia aliwaeleza Mabalozi kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ambapo alisema kuwa kuanzia Julai mpaka Novemba 2022 Miradi imeongezeka na kufika 132 yenye thamani ya dola bilioni 3.16 za Marekani ambayo ni ongezeko la asilimia 22.2 ikilinganishwa na idadi ya miradi iliyosajiliwa kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2021.

“Mfano mzuri waheshimiwa mabalozi, Serikali inatarajia kukamilisha ujenzi wa Bwawa la Nyerere mwezi Juni mwaka 2024 likiambatana na miradi mingine mikubwa” Dkt. Samia alibainisha

Kadhalika, Rais Dkt. Samia akatoa wito kwa mabalozi wanazowakilisha nchi zao kuungana na Serikali kuhamisha ofisi zao katika Makao Makuu ya Serikali Jijini Dodoma.

“Mnafahamu kwamba Dodoma ndiyo makao makuu rasmi ya nchi yetu na Serikali imehamia huko na tunachukua kila hatua kuhakikisha linakuwa Jiji la kisasa lenye huduma zote muhimu. Tunawaomba mfanye mipango ya kuhamia Dodoma ili muweze kunufaika na fursa mbalimbali ambazo Serikali inatoa kabla ya kumaliza wakati wake,” aliongeza Rais Dkt. Samia.

Post a Comment

0 Comments