SHULE YA SEKONDARI YASHINDWA KUPOKEA WANAFUNZI KWA KUKOSA CHOO.


Na James Jovin, Kibondo.

Shule mpya ya sekondari Bitale iliyoko wilayani Kibondo mkoani Kigoma mpaka sasa haijapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza kutokana na kutokamilika kwa ujenzi wa choo na vyumba vya madarasa kujengwa chini ya kiwango kinachotakiwa licha ya serikali kutoa shilingi milioni 180 kwa ajiri ya shughuli hiyo.


Kutokana na hali hiyo chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Kibondo kimefanya ziara ya kushitukiza na kukagua miundo mbinu ya shule hiyo ambapo wamekuta hali isiyolidhisha katika ujenzi wa vyumba vya madarasa ambayo yangesaidia kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa wakati

Mwenyekiti wa ccm wilaya ya Kibondo bw. Hamisi Tahilo ameonesha kusikitishwa na hali aliyoikuta shuleni hapo na kuagiza taasisi ya kupambana na rushwa kuhakikisha inawachukulia hatua watu wote waliohusika na uzembe uliojitokeza na kusababisha wanafunzi kuendelea kusomea katika shule jirani ya Misezero mpaka sasa.

Mwalimu Joseph Mgarura ambaye ni msimamizi mkuu wa mradi huo amekili kupokea fedha kiasi cha shilingi milioni 180 na kuanza shughuli ya ujenzi huo tangu mwaka jana na kuongeza kuwa mapungufu yaliyojitokeza si kwa lengo la ubadhilifu bali ni udhaifu wa fundi aliyepewa kazi hiyo

Kwa upande wake mhandisi wa ujenzi bw. Edwin Edward anabainisha changamoto mbali mbali zilizobainika katika mradi huo wa ujenzi wa shule mpya ya kata ya Bitale ikiwemo nyufa kwenye ukuta, rangi kubanduka pamoja na mchanganyo wa simenti usiofaa kulingana na maelekezo.

Nae diwani wa kata ya Bitale bw. Gerevazi Mpagaze pamoja na afisa mtendaji wa kata hiyo bw. Phinias Samizi wamekili kuwepo kwa changamoto hiyo na kwamba ilitokana na kutoshirikishwa katika mradi huo kwa kuwa shughuli nyingi zilikuwa zikifanyika kwa uficho hivyo kushindwa kubaini ubadhilifu uliokuwa ukifanyika

Kutokana na hali hiyo mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya kibondo katika ziara hiyo bw. Lyola Kitaronja ameitaka taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa kufanya uchunguzi wa kina na kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kuhusika na ubadhilifu wa mali hiyo ya umma.

Post a Comment

0 Comments