TAASISI YA MOYO JKCI YATAKIWA KUJIKITA KWENYE UTOAJI HUDUMA ZA MATIBABU YA MOYO KWA WATOTO

Na Mwandishi Wetu - Dar Es Salaam.
Uongozi wa Taasisi ya Moyo  Jakaya Kikwete (JKCI-Dar Group) umetakiwa kujikita kwenye utoaji wa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 15.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Afya Mhe. @ummymwalimu mara baada ya kutembelea Hospitali hiyo ambayo sasa ipo chini ya usimamizi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Jijini Dar Es Salaam.

“Hapa nataka tujikite kwenye matibabu ya moyo kwa watoto walio chini ya miaka 15 tusitoke kwenye huduma ya moyo kama ilivyokuwa malengo ya Taasisi ya Moyo JKCI” amesema Waziri Ummy Mwalimu akitoa agizo hilo kwa Uongozi wa Taasisi ya JKCI.

Amesema kuwa rufaa zote za watoto wenye matatizo ya moyo zinatakiwa kwenda JCKI Dar Group badala ya Taasisi ya Moyo JKCI iliyopo Muhimbili ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika eneo moja wakisubiri kupata huduma.

Waziri Ummy amesema kuwa Hospitali ya Dar Group ipo katika mazingira rafiki kufikika kwa wakazi wa Wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni lakini hata kwa wageni wanaofika katika Mkoa wa Dar Es Salaam kwa usafiri wa treni au anga hivyo kuagiza Hospitali hiyo kuboresha zaidi huduma zinazotolewa ili kuvutia watu kufika hapo kupata huduma.

Amesema kuwa agizo hilo haliathiri utolewaji wa huduma nyinginezo ambazo zinaendelea kutolewa ila mwelekeo wa Hospitali hiyo utajikita kwenye umahiri wa utoaji wa matibabu ya kibingwa ya moyo.

Aidha Waziri Ummy ameagiza pia Taasisi hiyo kusogeza zaidi huduma za matibabu ya kibingwa ya Moyo katika Kanda ya Ziwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Mbeya huku akiagiza kituo cha Morogoro kufungwa ili kuongeza nguvu katika Hospitali ya Dar Group pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato.

Post a Comment

0 Comments