WAANDISHI WA HABARI WAPIKWA UTEKELEZAJI WA MRADI WA SHULE BORA

Na Adela Madyane, Kigoma

Zaidi ya wanahabari 20 mkoani Kigoma wamepewa mafunzo ya namna ya kutoa elimu kwa jamii juu ya mradi wa shule bora wenye lengo la kuhakikisha elimu bora, jumuishi, endelevu na salama inapatikana kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa kuzingatia elimu kwa wote bila ubaguzi wa aina yoyote.

Mradi huo unaotekelezwa na serikali chini ya wizara ya habari na TAMISEMI kwa udhamini wa shirika la msaada la Uingereza UKaid utagusa mikoa tisa ya Tanzania bara inayojumuisha Kigoma, Rukwa, Katavi, Pwani, Tanga, Simiyu, Mara, Singida na Dodoma ambayo ni mikoa iliyobainika kuwa na changamoto zaidi katika sekta ya elimu.

Akizitaja baadhi ya changamoto za jumla zinazokwaminisha elimu bora kwa wote zitakazofanyiwa kazi na mradi huo David Mwamalasi, afisa elimu taaluma mkoa wa Kigoma amesema ni pamoja na upungufu wa vyumba vya madarasa, umasikini na upungufu wa walimu, huku kwa mkoa wa Kigoma changamoto kuu ikiwa ni mdondoko, ufaulu hafifu wa darasa la saba pamoja na watoto wa kike kuolewa mapema na kushindwa kuendelea na elimu ya sekondari.

Kwa upande wake kaimu katibu tawala mkoa wa Kigoma Paulina Ndigeza ambaye pia ni Afisa elimu mkoa wa Kigoma ameweka bayana kuwa Kigoma ni miongoni mwa mikoa kadhaa ambayo haijafanikiwa kupata ufaulu unaofikia angalau asilimia 90 kwa matokeo ya mitihani ya taifa ya darasa la saba.

Ndigeza amesema mkoa wa Kigoma umeendelea kukabiliwa na kundi kubwa la Watoto wanaofika hadi darasa la nne bila kujua kusoma na kuandika, huku masoko ya usiku na utumikishaji wa watoto katika biashara ndogo ndogo ikitajwa kuwa sababu kubwa ya wanafunzi wengi kutofanya vizuri shuleni na wengine kuacha kabisa shule.

“Ni asilimia 49 pekee sawa na watoto 60130 wanaomaliza darasa la saba kati ya wanafunzi laki moja wanaoandikishwa darasa la kwanza wanaomaliza darasa la saba, suala hili linatajwa kusababishwa na mambo mengi ya kijamii ikiwemo wananchi wengi kuwa na mitazamo hasi katika elimu” Amesema Ndigeza.

Naye Celestine Bukango ambaye ni mratibu wa mradi WA Shule Bora amesema mradi utajikita katika maeneo makuu manne ya ufundishaji, ujifunzaji, ujumuishi pamoja kuimarisha mifumo ya utaoji wa habari na takwimu kwa usahihi kutoka shuleni na kuchakatwa kwenda wizarani bila doa lolote ili kuhakikisha maeneo hayo yanawezeshwa kikamilifu ili kufikia lengo la mradi la kupata elimu bora.

Amesema mradi pia utahusisha wazazi, jamii, walimu, viongozi wa shule pamoja na taasisi za elimu kwa lengo la kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao sambamba na kutambua vikwazo vilivyopo katika jamii ili kuviondoa na kuongeza ubora wa elimu kwa watoto ili waweze kufika elimu ya juu.

Bukango amesisitiza kuwa mradi wa Shule bora unatarajia kutumia kiasi cha paundi za uingereza milioni 89 sawa na shilingi bilioni 271 ambazo zitatekelezwa hadi mwaka 2027 katika halmashauri 97 zenye shule zaidi ya 5000, wanafunzi 3,800,000 na walimu 5400.

Post a Comment

0 Comments