WILAYA YA KASULU YAKAMILISHA UJENZI WA NYUMBA ZA WATUMISHI WA AFYA


Na Emmanuel Matinde, Kigoma

Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, imefanikiwa kujenga na kukamilisha nyumba tano za watumishi wa hospitali ya wilaya kutokana na mapato yake ya ndani huku ujenzi wa nyumba nyingine tatu ukiendelea kwa lengo la kuwawezesha watumishi kukaa karibu ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za dharura kwa wananchi.

Wakati serikali ikiendelea kutatua changamoto mbalimbali za utoaji wa huduma za afya kwa wananchi nyumba za  watumishi ni moja kati ya changamoto zilizosalia hivyo kwa kubuni mpango wa makazi bora kwa watumishi, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu imepiga hatua muhimu katika kufikia lengo la serikali la utoaji wa huduma bora za afya.

Wananchi wa halmashauri hiyo wameguswa na hatua hiyo huku watumishi wa hospitali nao wakieleza nyumba hizo zitawasaidia kufanya kazi katika mazingira mazuri.

Hiyo ni awamu ya kwanza ya ujenzi ambapo Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Dr. Robert Rwebangira, amesema ujenzi wa awamu ya pili utakapokamilika nyumba zitakuwa na uwezo wa kutunza familia za watumishi 17 idadi ambayo inakidhi huduma za dharura kwa saa 24, huku Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye, akiipongeza halmashauri hiyo kwa kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suuhu Hassan.


Post a Comment

0 Comments