MIILI MIWILI YA WATOTO WALIOKUFA MAJI KIGOMA YAPATIKANA



 


 Na Mwajabu Hoza, Kigoma

Miili ya wanafunzi wawili kati ya wanne waliozama katika tukio la boti kupinduka lililotokea siku ya jana asubuhi katika mto luiche Mkoani Kigoma imepatikana leo asubuhi.

 

Zoezi la uokoaji wa Watoto hao limeendelea leo asubuhi baada ya siku ya jana kushindwa kufanikiwa, majira ya asubuhi na mapema miili hiyo imeanza kuonekana ikielea katika mto Luiche karibu kabisa na Ziwa Tanganyika.

 

Kaimu kamanda wa Zimamoto na uokoaji mkoani Kigoma Inspekta Jacob Chacha anasema majira ya saa nne asubuhi kati ya Mto Luiche na Ziwa Tanganyika walifanikiwa kupata miili miwili ya watoto ambao ni Tatu Sanaari mwanafunzi wa darasa la pili (8) na Ramadhani Nkwila (12) mwanafunzi wa darasa la tano.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Filemon Makungu anasema hadi sasa vikosi vya polisi na zimamoto  bado vipo katika maeneo ya ziwa Tanganyika na Mto Luiche wakiendelea kutafuta miili mingine ambayo hadi sasa haijaonekana.

 

Familia za marehemu zimefika katika hospiali ya rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni na kuitambua miili ambayo ilikuwa imehifadhiwa hapo kabla ya kulazwa katika nyumba yao ya milele ambapo wameeleza kusikitishwa na tukio lililojitokeza ikiwa waliiomba serikali kuwawekea daraja kwa kipindi kirefu.

 

Wamesema wanapendekeza serikali iweke mtumbwi wa kuweza kuwavusha wakati jitihada zingine zikiendelea kuchukuliwa za ujenzi wa daraja ili kuondoa changamoto ya vifo kwa wakazi wanaoishi maeneo ya mwambao wa mto huo.

 

Mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye naye alifika hospitali hapo ambapo kabla ya kutoa salama za mwisho kwa marehemu akatoa pole kwa wafiwa na kueleza serikali kugharamia mazishi hayo.

 

“Serikali itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha inaungana na familia za marehemu katika kuwapumzisha kwa heshma na kwa staha watoto ambao wamefariki”

Tatu Sanaari (8) mwanafunzi wa darasa la pili na Ramadhani Nkwila (12) wa darasa la tano ambao miili yao imeonekana, wamezikwa leo alasiri huku zoezi la kutafuta miili mingine miwili ya Zabibu Jumanne na Ashura Haruna likiendelea kufanywa katika eneo lote la mto Luiche na Ziwa Tanganyika.


Ikumbukwe kuwa jana ijumaa watoto sita ambao ni wanafunzi wa shule ya Msingi Kagera walikuwa wakivuka mto Luiche uliopo Manispaa ya Kigoma Ujiji kuelekea shuleni ambapo mtumbwi waliokuwa wakitumia ulipigwa na dhoruba na kupinduka na kusababisha watoto wanne kupotea majini na wawili kuokolewa.


Hata hivyo hii leo kati ya watoto wanne waliopotea wawili wamepatikana wakiwa wamefariki na tayari shughuri za mazishi zimeshafanywa na familia zao kwa kushirikiana na serikali.

 

Post a Comment

0 Comments