MWALIMU AFARIKI BAADA YA KUSHAMBULIWA NA KUNDI LA NYUKI


Na Adela Madyane, Kigoma.
Mwalimu wa shule ya msingi Mambo iliyopo Ujiji  aliyekuwa mkazi wa eneo la Shia mtaa wa Masangalubabi kata ya Mwasenga Manispaa ya Kigoma Ujiji Deogratius Ndogoye (51) amefariki dunia baada ya kushambuliwa na kundi la nyuki walioko kwenye mti wa mwembe maeneo ya nyumbani kwake.

Nyuki hao walimvamia mwalimu huyo alipokuwa akielekea kwenye matembezi na kupita kwenye njia iliyopo pembezoni mwa mwembe huo muda mchache baada ya watoto waliokuwa wakitoka shuleni kutupa mawe juu ya mwembe huo na kusababisha nyuki kuanza kuzagaa wakitafuta anayewachokoza na ndipo walipomvamia na kuanza kumshambulia hali ambayo ilisababisha kupoteza maisha.

Akizungumza tukio hilo, mtoto wa marehemu Emily Ndogoye amesema alikuwa ndani amejipumzisha majira ya saa 11 jioni ambapo ghafla mdogo wake alimuita na kumuomba aende akamuokoe baba yake aliyekuwa akiomba msaada kutokana na kushambuliwa kundi la nyuki chini ya mwembe.

“Nilikuta nyuki wameenea mwilini mwa baba yangu, nikajitahidi kumvuta miguu yake ili kumuokoa, sikufanikiwa kwakuwa wale nyuki walitoka kwake wakanivamia mimi, nikakimbia na kuvua shati, walinin’gata sehemu tofauti za mwili nikadondoka kwa maumivu, wakaja watu wakanipeleka kwenye moto na kisha kunipeleka hospitali kwaajili ya kupata huduma za kuondoa sumu mwilini, lakini muda wote huo baba yangu alikuwa ameshafariki dunia” amesema Ndogoye

Naye Sinjelo jirani wa marehemu amesema walifanya jitihada za kuyaokoa maisha yake lakini hawakufanikiwa kwakuwa nyuki walikuwa wengi na wakashindwa namna ya kuwadhibiti.

Vilevile jirani Victoria James amesema alijaribu kwenda kumuokoa ila alishindwa kwakuwa nyuki walimvamia pia na ndipo alipoamua kukimbilia ndani ili kunusuru maisha yake na kupiga kelele kuomba msaada zaidi kwa watu ambao nao walijitokeza japo walishindwa kuokoa maisha yake

Kwa upande wa Shaban Ndimugoye muokoaji wa mwili wa marehemu amesema alipopata taatifa za tukio alikimbia nyumbani kwake kuchukua mafuta ya petroli pamoja na majani ili kuwasha moto kwa lengo la kuwafukuza nyuki ili kufanya uokoaji bila madhra zaidi kutokea.

“Nyuki walianza kunishambulia mita 15 kutoka alipokuwa amelalala marehemu, nilimwaga petroli na kuwasha moto na kisha nikakimbia alipokuwa amelala nikambeba, ili kujikinga na moto niliwaomba watu waliokuwepo kuendelea kuwasha moto nyuma yangu na ndipo nilipofanikiwa kumfikisha nyumbani kwake ambapo tulisitiri mwili wake na kisha kupiga simu polisi ambapo walituelekeza kuupeleka katika hopitali ya rufaa ya Maweni” amefafanua Ndibugoye

Akielezea Michael Bisaki mjomba wa marehemu amesema alipata taarifa za ajali hiyo alipokuwa kanisani na kuelekea hospitali ambapo alikuta mwili wa marehemu ukiwa unahifadhiwa katika jokofu na kusema kuwa alikuwa amevimba uso na miiba ya nyuki kuenea kuanzia kichwani mpaka tumboni.

Mwenyekiti mstaafu wa kitongoji cha Masanga Lubabi Aron Nyabakali amesema tukio hilo sio la kwanza katika eneo hilo, mara ya kwanza nyuki hao walivamia mifugo ambapo mbwa wawili walikufa na kuziomba mamlaka za maliasili kufanya harakati za kuwatoa nyuki hao na ikibidi mwembe huo ukatwe kwaajili ya usalama wa wananchi

Akizungumzia tukio hilo Felix Kiphumu afisa maliasili na mazingira ya manispaa ya Kigoma Ujiji amesema jamii inapaswa kupewa elimu ya namna ya kujilinda na kuiasa kuacha vitendo vya kuwachokoza nyuki na wanyama wengine kwani wakikasirika wanachukua hatua za kujihami kwa kufanya mashumbulizi yaletayo madhara kwa jamii.

Marehemu mwalimu Deogratius amecha mke na watoto watatu.

Post a Comment

0 Comments