MWILI MWINGINE WAPATIKANA MTO LUICHE KATIKA TUKIO LA WATOTO KUZAMA

Na Diana Rubanguka, Kigoma
Jumla ya miili iliyopatikana hadi sasa imefikia mitatu baada ya Boti liliokuwa linavusha wanafunzi wa shule ya msingi Kagera  kuzama katika mto Luiche uliopo Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma baada ya mwili mwingine mmoja kupatikana katika kingo za mto huo mapema February 28, 2023.

Hayo yameelezwa na Kaimu Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Kigoma, Jacob Chacha, ambapo  amesema mwili huo uliopatikana umetambulika kwa jina la Ashura Ramadhani wenye umri wa miaka 8.

Chacha amesema mwili huo umepatikana majira ya saa tano asubuhi mara baada ya kupata taarifa kutoka kwa mvuvi aliyefahamika kwa jina la Juma Kabiligi aliyeuona mwili wa mwanafunzi huyo katika kingo za mto Luiche ambao unamwaga maji yake katika ziwa Tanganyika na taarifa kwa timu yao inayofanya shughuli ya utafutaji wa miili hiyo.

"Baada ya kupokea taarifa kutoka kwa mvuvi kuwa kuna mwili mmoja umepatikana, niliijuliasha timu yangu ambapo  walienda eneo tukuo na kuuchukua mwili huo na kuupeleka katika hospitali ya rufaa ya Mkoa Maweni kwaajili ya kuhifadhiwa ili baadae taratibu nyingine zifuate" anasema Chacha.

Aidha  baada ya kuufikisha katika hospitali hiyo waliweza kufanya mawasilianao na wazazi ili waweze kwenda na kufanya utambuzi wa mtoto huyo, ambae alitambuliwa kuwa ni Ashura Ramadhani aliyekuwa anasoma darasa la kwanza.

Kwa upande wake Baba mzazi wa mwanafunzi huyo,  Ramadhani Haruna amesema wanaishukuru serikali kwa kuendelea kuwa nao bega kwa bega kuhakikisha miili ya watoto wao inapatikana na kwenda kuwastiri katika nyumba zao za milele.

Hata hivyo jitihada za kuendelea kumtafuta mwanafunzi aliyesalia kati ya wanne waliozama baada ya kupatikana kwa miili mitatu zinaendelea katika kingo za mto huo na ziwa Tanganyika ambapo pia mwanafunzi huyo ametambuliwa kwa jina la Zabibu Jumanne licha ya kuwa bado hajapatikana.

Naibu Kamanda Chacha amewataka wananchi na wavuvi wanaofanya kazi katika maeneo hayo watakapoona mwili watoe taarifa kama walivofanya awali  ili waweze kukamilisha zoezi hilo.

Februari 24,2023 majira ya saa 1:30 asubuhi wanafunzi wanne kati ya sita wa  shule ya msingi Kagera walizamana katika mto luiche baada ya mtumbwi waliokuwa wakitumia kuvuka kupinduka na kuzama majini wakati wakienda shule huku wanafunzi wawili wakinusurika kifo.

Ilipofika Februari 25,2023 jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Kigoma kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kuipata miili miwili ya wanafunzi hao kati ya minne ambao ni Ramadhani Nkwila na Tatu Omari  katika makutano ya ziwa Tanganyika na mto luiche ikiwa inaelea juu ya maji ambapo miili hiyo  ilizikwa siku hiyo.

Post a Comment

0 Comments