VIONGOZI WATAKIWA KUTAFSIRI MKATABA WA LISHE KWA WANANCHI

Na Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Angellah Kairuki amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji na Vitongoji  pamoja na wataalam wa Afya nchini kuhakikisha wanautafsiri Mkataba wa lishe  kwa wananchi ili uweleweke 

Ameyasema hayo leo Februari 23, 2023 Jijini Dar-es-salaam wakati alipowasili  kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kuanza ziara yake ya Kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa  kwenye Majimbo ya Ukomga, Segerea na  Kigamboni.

Amewataka viongozi hao kuhakikisha wanawashirikisha wataalam kwenye ngazi ya jamii ili waweze kuelewa kwa kina Mkataba huo na kuwa mabalozi wa kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa lishe nchini

Amewataka kuhakikisha kuwa mikutano inayofanyika kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa suala la Mkataba wa lishe uwe ndio agenda kuu lengo likiwa kila mwananchi aweze kujua umuhimu wa lishe na kupunguza udumavu wa watoto nchini.

“Ni muhimu tukashuka hadi katika ngazi ya mitaa kuhakikisha tunatoa elimu ya kutosha kuhusu Mkataba wa lishe, kwa kufanya hivyo kutasaidia kila mmoja kujua umuhimu wa lishe nchini” amesisitiza Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki amewaagiza viongozi hao kuhakikisha Mkataba wa Lishe unajulikana na kueleweka kwa wananchi ili kuweza  kujua hali ya uduni wa lishe, udumavu lengo likiwa ni kupima utekelezaji wa mkataba huo 

Aidha ameupongeza Mkoa wa Dar-es-salaam kwa kutekeleza Mkataba wa lishe kwa asilimia 95 lakini amewataka kuhakikisha wanautafsiri mkataba huo kwa wananchi ili uweze kueleweka na kupata matokeo yanayotegemewa na Serikali.

Vilevile Waziri Kairuki amewaagiza viongozi hao kuhakikisha wanafanya utafiti wa kina kuhusu mawakala wanaopatiwa POS kwa ajili ya kukusanya mapato kwenye Halmashauri kwa kuwa wengi wao huzizima na kutozisajili na hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa mapato

Amewataka kuongeza usimamizi na kujiridhisha  kwenye upatikanaji wa  Mawakala wanaoteuliwa kwa ajili ya kukusanya mapato ya Halmashauri  pamoja na  kuangalia kamisheni zinazotolewa kama ni kiwango sahihi na ndicho kinachotakiwa

Post a Comment

0 Comments