WAGANGA WAKUU WA MIKOA NA WAGANGA WAFAWIDHI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA USHIRIKIANO

Na Mwandishi Wetu, Dodoma 
Waganga wakuu wa Mikoa (RMOs) pamoja na Waganga wafawidhi wa Hospital (MOI) wametakiwa kufanya kazi kwa kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao ili kuwezesha kutoa huduma bora za afya kwa wananchi. 

Wito huo umetolewa leo na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe wakati akifungua kikao kinachohusisha Bohari ya Dawa (MSD) na Mfuko wa Taifa wa Bima (NHIF) pamoja na Waganga Wakuu wa Mikoa, Halmashauri na Waganga Wafawidhi wa Hospitali na vituo vya afya unaofanyika Jijini Dodoma.

"Kama muswada wa bima ya afya kwa wote ukipitishwa na Bunge tuwe tumejiimarisha katika utoaji wa huduma kuanzia mapokezi hadi mteja anapomaliza kupata huduma, ninashangaa sana kusikia baadhi ya Waganga Wakuu wa Mikoa na Waganga wafawidhi hawaelewani. Hii inapelekea kutoa huduma duni kwa wananchi na kutofikiwa lengo la Serikali". Amesema Dkt. Shekalaghe.

Aidha, Dkt. Shekalaghe amewataka viongozi wa mfuko wa bima ya afya (NHIF) kufuatilia udanganyifu unaofanywa na baadhi ya vituo vya Afya pamoja na kuwasilisha madai ya mfuko huo kwa wakati.

Pia, ameitaka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kusambaza dawa mapema katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na kuwa na mawasiliano ya haraka pindi wanapopata changamoto.

Mwisho. Dkt. Seif Shekalaghe amewahakikishia Watanzania kuwa huduma bora zimeanza kutolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya hivyo kuwatoa wasiwasi pindi bima ya afya kwa wote itakapopitishwa wasisite kujiunga.

Post a Comment

0 Comments