WATU WAWILI WANUSURIKA KIFO BAADA YA KUSHAMBULIWA NA KIBOKO MTO LUICHE MKOANI KIGOMA.

Na Diana Rubanguka, Kigoma.
Mtu mmoja mkazi wa kata ya Kagera iliyopo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji amelazwa katika Hospital  ya rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni baada ya kujeruhiwa na Kiboko wakati akiwa katika shughuli za uvuvi katika eneo la makutano ya mto Luiche na Ziwa Tanganyika.

Akizungumza hospitalini hapo mmoja wa majeruhi Ngwanije Mdyanko amesema, tukio hilo  lilitokea wakati wakiwa katika shughuli za uvuvi ambapo kiboko akiwa na mtoto wake waliibuka na kuanza kuwakimbiza na wakati wakiwa katika harakati za kujiokoa Kiboko huyo alifanikiwa kubinua mtubwi na kumjeruhi sehemu ya Goti na kaka yake Ayubu Mdyanko sehemu ya  mgongoni.

"Ilikua saa nane usiku tukiwa wawili mimi na kaka yangu, tulikua tunatembea na mtubwi juu ya maji tukakutana na kiboko mama na mtoto, wakati tunajihami kukimbia kwenye maji mengi mama alitufikia na kuubinua mtubwi ambapo kaka alikwaruzwa mgongoni na mimi nikanyofolewa nyama juu ya goti.

Baada ya kupambana kujiokoa tulijikuta tukiwa mbali na mtubwi, ikatulazimu kukaa katika kichaka hadi ilipofika asubuhi ndipo tukapata msaada wa  kasia kutoka kwa wavuvi waliopita eneo hilo na kufanikiwa kufika nchi kavu" Anasema Mdyanko

Mdyanko ameongeza kuwa  baada ya majeraha hayo walifika katika hospital ya Ujiji ambapo waliambiwa tatizo ni kubwa hivyo hawawezi kutoa matibabu na kuwahamishia katika hospital ya rufaa ya Mkoa wa Kigoma maweni ambapo wanaendelea na matibabu.

Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo  Gregory Kebelezo anasema tukio hilo siyo la kwanza kwa Viboko kuua na kujeruhi wananchi wanaojihusisha na shughuli za uzalishaji katika eneo hilo.

"Baada ya kupokea taarifa hizo nilitoka taarifa kwa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa, ambapo zoezi la kutafuta miili lilisitishwa kwa muda na kuendelea asubuh ya leo  februari 27, 2023" alieleza Kebelezo.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la zimamoto na uokoaji Jacob Chacha amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa baada ya kupokea taarifa hizo walisitisha uokoji wa miili miwili iliyosalia katika ajali ya kuzama kwa Boti katika mto huo mwishoni mwa juma lililopita kutokana na wanyama wakali wakiwemo Mamba na Viboko waliojeruhi wavuvi usiku wa kuamkia jana.

Kamanda Chacha amewataja majeruhi hao kuwa ni Ngwanije Mdyanko mwenye umri wa miaka 20 na Ayubu Mdyanko.

Nae Mganga mfawidhi wa Hospital ya rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni Dkt. Stanley Binagi amekili kumpokea majeruhi huyo hospitalini hapo jana asubuh na kusema kuwa anaendelea na matibabu.

Post a Comment

0 Comments