WAZIRI MKUU APIGA MARUFUKU MATUMIZI YA KIPIMO CHA BIDOO

Na Mwandishi Wetu, Kigoma
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Tobias Andengenye kwa kushirikiana na SIDO wahakikishe wanaingiza sokoni vipimo rasmi vya kupimia mafuta ya mawese na kuachana na vipimo vya asili maarufu kama BIDOO ambacho kimekuwa kikiwanyonya wakulima.
 
Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Februari 27, 2023) alipotembelea Viwanda vya Kukamua mafuta ya mawese, kukausha Mbegu za Michikichi na  Kiwanda cha kusindika mafuta ya mawese cha Trolle Messle, Mjini Kigoma.
 
Mheshimiwa Majaliwa ametoa agizo hilo baada ya mbunge wa kigoma kaskazini Assa Makanika kuomba Serikali kuagiza kuingizwa sokoni kwa vipimo vya mafuta ya Mawese badala ya kutumia vipimo vya Bidoo
 
“Mheshimiwa Waziri Mkuu mkulima amekuwa akipunjwa sana kutokana na matumizi ya kipimo cha Bidoo, mnunuzi anaweka maji moto kwenye dumu na linatanuka badala ya kuingiza lita 20 linaingiza lita 25 na mkulima anapewa fedha za lita 20” Amesema Mbunge huyo
 
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Bidoo haikubaliki na haipo kwenye sheria hivyo mfanyabiashara kutumia vipimo hivyo ni kumnyonya mkulima “haiwezekani mnunuzi alipe fedha ya lita 20 halafu unapewa lita 25 na unamlipa mkulima fedha ya lita 20, kwasababu ya kutumia kipimo cha Bidoo”
 
“Mkuu wa Mkoa hili ni lako wewe na wakuu wa wilaya, nendeni kwenye masoko yote yenye bidhaa ya mawese angalieni vipimo vinavyotumika, mkikuta Bidoo zikamateni na wananchi msikubali kupima mafuta kwenye Bidoo, ukiona mnunuzi ana kipimo hicho toeni taarifa”
 
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu ameiagiza SIDO kuendelea kubuni teknolojia nzuri na rahisi ya kukamua mafuta ya mawese ili kuwawezesha wananchi kuwa na uwezo kuzalisha mafuta mengi na bora
 
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan  ameiwezesha SIDO kwa kutoa fedha ili wabuni mitambo ya kisasa ya kukamua mafuta ya mawese mpaka kwa asilimia 100 ili kuachana na teknolojia ya zamani na kumuwezesha mkulima apate mafuta mengi ili ajikwamue kiuchumi”

Post a Comment

0 Comments