WAZIRI MKUU AZIGEUKIA SEKTA ZINAZOHUSIKA NA MAAFA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka sekta zote zinazohusika na utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa, idara au taasisi zenye jukumu la kisheria la kutekeleza kazi hiyo zihakikishe zinawajibika kikamilifu katika kushughulikia vizuri pindi maafa yanapotokea.

Amesema pamoja na uwepo wa sera na sheria ya usimamizi wa maafa na nyaraka alizozindua ambazo zimelenga kuimarisha mifumo ya uwajibikaji kwa kila sekta, ushirikiano unahitaji katika kutekeleza afua za ustahimilivu na kuzuia maafa.

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Februari 9, 2023) wakati akizindua nyaraka za usimamizi wa maafa katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma. Nyaraka zilizozinduliwa ni Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa (2022).

Nyaraka nyingine ni Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano Wakati wa Maafa (2022), Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja (2022-2027), Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa (2022-2027) na Mwongozo wa Taifa wa Kupambana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu (2022).

Amesema miongozo na mipango hiyo ya usimamizi wa maafa inatoa jukumu kwa wizara, Serikali za Mitaa, hivyo taasisi pamoja na wadau wengine kuandaa mipango kazi na taratibu za usimamizi wa maafa pamoja na namna ya kushughulikia dharura pindi inapojitokeza.

Waziri Mkuu amesema nchi bado inao uwezo wa kudhibiti majanga yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu, hivyo wahusika wawajibike katika kuelimisha umma wa Watanzania namna ya kukabiliana na majanga na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa nyaraka hizo.

“Nitoe rai kwa Watanzania wenzangu, tuwe sehemu ya watendaji wakati wa dharura zinapojitokeza badala ya kusubiri tuanze kulaumu. Wale wenye nguvu na uwezo wa kusaidia wajitokeze kuunga mkono jitihada za Serikali badala ya kuwa watazamaji mfano ilipotokea ajali ya ndege wananchi walijitokezakusaidia.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali kwa upande wake itaendelea kuimarisha mbinu na mikakati ya makusudi ya udhibiti wa athari zitokanazo na maafa pamoja na usimamizi wa utekelezaji wa sera, sharia na mikakati ya usimamizi wa maafa.

Post a Comment

0 Comments