HALMASHAURI NUFAIKA NA FEDHA ZA CSR ZATAKIWA KUWASILISHA TAARIFA

Na Mwandishi Wetu, Mara
Kamati ya Kudumu ya Bunge Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI) imezitaka Halmashauri  zote nchini  zinazonufaika na fedha za uwajibikaji (CSR) kuwasilisha  taarifa ya matumizi ya  fedha hizo wakati wa kuwasilisha bajeti zao kwa  Mwaka 2023/2024.

Agizo hilo limetolewa  Machi 15,2023 na Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI) Mhe. Denis Londo  baada ya kubaini mashaka ya matumizi  ya fedha hizo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

" Haiwezekani Halmashauri inapata  Bil. 7 kwa mwaka jana  na bado haionekani imefanya kazi gani, hiyo fedha tungeweza kujenga vituo vingapi vya afya, Sasa sio Halmahauri hii pekee  Halmasahuri zote  nchini ziwasilishe taarifa za matumizi ya fedha hizo "Amesema Mhe. Londo

Sambamba na hilo  ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuimarisha usimamizi na kuongeza kasi katika utekelezaji wa ujenzi wa jengo la utawala ili jengo hilo liweze kukamilika  na kuanza kutumika.

Aidha Kamati hiyo  imetoa pongezi kwa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini ( TARURA)  Mkoa wa Mara kwa kusimamia vizuri ukarabati wa  barabara ya Kwangwa-  Mkirira  na Mwisenge - Nyamlasa.

" Kamati imefurahishwa na ujenzi unaoendelea hapa utekelezaji unaridhisha  sana hongereni, na huyu mkandarasi  apewe kazi nyingine maana viwango vyake  vinaridhisha" Amebainisha  Londo

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( OR-TAMISEMI) Mhe. Deogratius Ndejembi  amesema kuwa  atazungumza na SUMA JKT ili kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazokwamisha ukamilishaji wa ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Tarime.

Post a Comment

0 Comments