RAIA ZAIDI YA 2600 KUTOKA CONGO DR WAINGIA MKOANI KIGOMA WAKIOMBA HIFADHI

Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Takribani wakimbizi 2600 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wapo mkoani Kigoma wakiomba hifadhi kufuatia vita vinavyoendelea nchini kwao.

Baadhi ya wakimbizi hao akiwemo Msafiri Goliathi wamesema sababu ya kuondoka nchini kwao na kukimbilia Tanzania ni kutokana na hofu ya kupoteza maisha kutokana na vita huku wengine wakisema wamepoteza wazazi wao.

"Nilipewa taarifa kuwa baba yangu ameuwawa kwa kuchomwa moto nami nikaingiwa hofu ikabidi nikimbilie huku ili kunusuru maisha na kupata chakula" amesema Goliathi.

Mkurugenzi wa Idara ya wakimbizi Sudy Mwakibasi amesema wameanza kuwapokea raia hao kuanzia tarehe 5 March mwaka huu na kusema kuwa raia wengi wameeleza kuwa wanatokea katika maeneo ya Kivu kusini na Kaskazini mwa Goma na mji wa Ben.

Awali akizungumzia kuhusu uwepo wa raia hao kutoka Nchini Kongo Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye amewataka wananchi kutopokea mgeni kinyemela na badala yake wafuate taratibu huku akiwataka Raia hao kutoka kuishi kwa kuzingatia misingi na taratibu za nchi ya Tanzania wakati wakisubiri kujua hatma yao.

 Hii si mara ya kwanza kwa Nchi ya Tanzania kuwapokea raia kutoka nchini Congo ambao wanakuja kuomba hifadhi hata hivyo Idara ya wakimbizi imesema imejipanga vyema kwa ajili ya kuwapokea na mpaka sasa mahojiano yanaendelea kwa ajili ya taratibu zingine ikiwemo kuwapeleka kambi ya Nyarugusu. 

Post a Comment

0 Comments