REJESHENI MIKOPO WENZENU WAPATE KUKOPA –KAMATI YA LAAC

Na Mwandishi Wetu, Mtwara
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imetoa wito kwa vikundi vinavyopatiwa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kurejesha mikopo waliyokopeshwa ili kutoa nafasi kwa vikundi vyengine kuweza kukopa.

Hayo yamebainishwa  leo Machi 28, 2023 katika  ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa,  Halmashauri ya Mji Nanyamba Mkoani Mtwara walipotembelea  Kikundi cha Vijana cha Kimbilio kinachojishughulisha na uzalishaji wa chaki.

Mwenyekiti wa Kamati  hiyo Mhe. Halima Mdee (Mb) amesema, fedha zilizotolewa na Serikali sio kwa ajili ya kutolewa bure bali ni kuwezesha jamii kujiendeleza kichumi katika kujitafutia riski na kujikwamua kimaisha, hivyo ni jukumu la kila kikundi kilichopatiwa mkopo kuweza kurejesha ili  kuwapa nafasi vikundi/jamii nyingine kuweza kukopeshwa.

“Tumekuja  kujiridhisha kama kweli mlipewa mkopo na  mnajishughulisha na biashara mliohitaji ”amesema Mhe.Mdee

Akielezea lengo la ziara hiyo  ni kutaka kujua maendeleo ya shughuli zinazofanywa na vikundi hivyo na kuwataka kuhakikisha wanarejesha  mkopo kwa wakati  ili wengine waweze kupatiwa mikopo hiyo.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kikundi Katibu wa Kikundi cha Vijana cha Kimbilio Bw. Shaibu Gobosi amesema wanaishukuru Serikali kwa kuwapa  nafasi na kuwaamini  kuwakopesha sh. mil. 38,000,000.00 ambapo wemeweza kuanzisha kiwanda cha uzalishaji wa chaki na kununua mashine na malighafi.

Gobosi ameeleza kuwa, pamoja na mkopo huo ameiomba Serikali kuisapoti  biashara yao iwe ni yenye kuleta tija na maendeleo kwa familia yao lakini jamii kwa ujumla.

Aidha, amesema Serikali ikiendelea kuunga  mkono jutihada zao italeta chachu kuimarisha vikundi vingine vya vijana wajasiriamali ndani na nje ya Halmashauri ya Mji Nanyamba.

Pia ameiomba Serikali kuwekeza  kwenye ununuzi wa chaki hizo katika kiwanda hicho ili kuwapa ari  ya kufanya kazi na kuongezeka  kipato.

Post a Comment

0 Comments