WAGANGA WAKUU WA MIKOA NA HALMASHAURI ONGEZENI KASI YA UTOAJI CHANJO KWA WATOTO CHINI YA MIAKA MITANO.

Na Mwandishi Wetu, Tabora
Serikali kupitia Wizara ya Afya imewataka Waganga wakuu wa Mikoa na Halmashauri nchini kuhakikisha watoto wote chini ya miaka mitano katika maeneo yao wanapatiwa chanjo ili kuepuka magonjwa ya milipuko. 

Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe leo Mkoani Tabora wakati alipofanya ziara katika kituo cha Afya Maili Tano na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete Tabora kwa lengo la kujionea hali ya utoaji chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano na ubora wa huduma.

Dkt. Grace amewataka wataalamu wa afya kila wanapo kwenda kufanya huduma za mkoba lazima na huduma ya utoaji chanjo iwepo  ili kuongeza kasi katika utoaji chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano.

“Taarifa ya Mganga Mkuu wa Mkoa imeonyeshq kuna watoto 48,000 mkoani Tabora hawajafikiwa kupatiwa chanjo na wengine wamepata  dozi ya chanjo badala ya mbili, hivyo ni wajibu wetu kuwafikia na kuhakikisha tunawapatia chanjo ili kuokoa maisha yao”, maagizo haya yanawahusu Waganga wakuu wa Mikoa na Halmashauri zote"ameeleza Dkt. Grace

Amesema kuwa hakuna sababu ya msingi watoto kuugua au kupoteza maisha kwa magonjwa ambayo yanazuilika kwa chanjo.

Hivyo Dkt. Grace amesisitiza wataalamu wa afya kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano pamoja na matumizi sahihi ya kadi ya kliniki ya mtoto .

Katika Hatua nyingine  Dkt. Grace ametoa pongezi kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete Tabora pamoja na watumishi wa kituo cha Afya cha Maili Tano kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuwatumikia Watanzania katika kutoa Huduma za afya

Vile vile Dkt. Grace amepata nafsi ya kuongea na wananchi waliofuata huduma katika hospitali ya ya Rufaa ya Mkoa Kitete na kuwasisitiza wananchi hao kujiunga na Bima ya afya ili kujihakikishia uhakika wa matibabu pale wanapougua. 

Akizungumza Dkt. Grace amempongeza Mlinzi wa Wodi ya Wazazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kitete Tabora,  Bi. Hamida Iddy Fundi kwa kufanya vizuri katika swala zima la huduma kwa mteja.

Post a Comment

0 Comments