WIZARA YA AFYA YATAKIWA KUONGEZA UFUATILIAJI WA MAGONJWA YA MLIPUKO

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Mhe George Simbachawene, ameitaka Wizara ya Afya kuongeza ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu ili  kuhakikisha unadhibitiwa usisambae nchini hususani katika maeneo ambayo yanapata milipuko ya mara kwa mara.

Waziri Simbachawene ameyasema hayo leo Machi 22, 2023 Jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mpango Shirikishi wa  Taifa wa kuzuia na kukabiliana na kipindupindu wa mwaka 2023-2027 wenye kauli mbiu isemayo "Ushirikiano wa Kisekta ni mkakati sahihi wa kuzuia, kukabiliana na kutokomeza kipindupindu nchini Ifikapo mwaka 2030".

"Sisi sote tuna jukumu katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko ikiwemo ugonjwa huu wa kipindupindu ambapo chanzo chake kikubwa ni uchafu na matumizi ya maji yasiyo salama hivyo niwaombe wizara ya afya kuhakikisha wanapeleka nguvu katika maeneo yaliyoathirika sana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ili kubaini chanzo na kuweka mikakati ya kutokomeza". Amesema Waziri Simbachawene 

Pia amezitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI kushirikiana na Mamlaka za maji mijini na vijijini kuhakikisha wanadhibiti matumizi ya maji taka na kuhakikisha maji yanayotumika ni salama na kudhibiti pia maji taka yasitiririke katika mazingira na makazi ya watu ili kuepukana na milipuko ya magonjwa ikiwemo ugonjwa wa kipindupindu.

Hata hivyo, ameitaka ofisi hiyo  kuongeza kasi katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya vyoo bora, matumizi ya maji safi na salama, kutotiririsha maji taka hovyo, kunawa mikono baada ya kutoka chooni na kabla na baada ya kula ili kupunguza milipuko ya magonjwa ikiwemo kipindupindu. 

"kipindupindu ni ugonjwa wa aibu ambao haupaswi kutajwa katika nchi yetu ambayo imepiga hatua kubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Miundombinu na sekta zingine hivyo ni aibu sana kuendelea kuwa na tishio la ugonjwa huu wa aibu". Ameongeza Simbachawene 

Naye Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa kwa mwaka 2015 Tanzania ilikuwa na visa vilivyoripotiwa vya ugonjwa wa kipindupindu 12,985 wakati kwa mwaka wa 2022 visa vilivyoripotiwa ni 537

Post a Comment

0 Comments