SERIKALI YAANDIKA HISTORIA UJENZI WA BARABARA MKOANI KIGOMA

Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Serikali imeandika historia mkoani Kigoma ambapo imetoa kiasi cha zaidi ya bilioni 567 kwa ajili ya miradi tisa ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 420 kwa kiwango cha lami mkoani humo.

Ujenzi wa barabara hizo zitawezesha mkoa huo kuunganishwa kwa barabara za kiwango cha lami na mikoa ya Tabora, Katavi na Rukwa pamoja na nchi za jirani za Rwanda, Kongo na Burundi na hivyo kurahisisha shughuli za usafiri na usafirisha na hivyo kukuza uchumi wa mkoa huo na nchi kwa ujumla.

Hayo yameelezwa na Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoani Kigoma Mhandisi Narcis Choma, wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya miradi inayotekelezwa na wakala huo kwa wanahabari waliofanya ziara Mkoani humo ili kuona maendeleo ya miradi inayotekelezwa na Serikali hususani ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja.

Mhandisi Choma ameeleza kuwa hadi sasa zaidi ya kilometa 100 zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami na nyingine zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake.

Ameitaja miradi hiyo ikiwemo ni ujenzi wa barabara ya Kazilambwa (Tabora) - Chagu (Kigoma) (km 36) umefikia zaidi ya asilimia 80, Malagarasi – Ilunde Uvinza (km 51.1) umefikia asilimia 31 na ujenzi wa barabara ya Kibondo – Mabamba mpakani mwa Burundi (km 47.93),

Barabara nyingine ni Manyovu – Kasulu – Kibondo – Kabingo (km 260.6) ambayo imegawanyika katika sehemu nne nazo ni Kasulu – Manyovu na viunganishi vyake (km 68.25) umefikia asilimia 47.12, Kanyani – Mvugwe (km 70.5) umefikia asilimia 54, Mvugwe – Njiapanda (km 59.36) umefikia asilimia 66.3, Nduta  - Kabingo (km 62.5) umefikia asilimia 78.5 pia TANROADS inatekeleza ujenzi wa barabara sehemu ya Njiapanda ya Nduta Kibondo Mjini (km 25.9) ambayo umefikia asilimia 57.3.

Aidha, ameeleza kuwa miradi hiyo imeweza kutoa fursa za ajira zaidi ya vijana wazawa 1,500 wanatoka katika wilaya zinazopita mradi huo mkoani humo.

Kuhusu manufaa mengine ya miradi hiyo kwa jamii inayozunguka, Mhandisi Choma ameongeza kuwa katika mradi huo kumepatikana utoaji huduma za kijamii ambapo zaidi ya shilingi Bilioni 21 zitatumika katika miradi ya nyongeza katika Wilaya za Buhigwe, Kasulu na Kibondo.

Post a Comment

0 Comments