SERIKALI YAENDELEA KUWEKEZA KATIKA MIRADI MBALIMBALI ITAKAYOCHANGIA AJIRA KWA VIJANA

Na Mwajabu Hoza , Kigoma.
MKUU wa wilaya ya Kigoma Salum Kalli amesema serikali imeendelea kuwekeza katika miradi mbaimbali ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa ndege, meli, ujenzi wa miundombinu ya barabara , huduma za afya pamoja na ujenzi vyumba vya madarasa miradi ambayo itachangia ongezeko la ajira kwa vijana wanaohitimu vyuo mbalimbali nchini.

Kauli hiyo imetolewa wakati akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Nyarubanda iliyopo wilaya ya Kigoma lengo likiwa ni kuwapa matumaini, hamasa na kuwatia moyo wanafunzi wa kidato cha sita wanaotarajia kuanza mitihani yao Mei 2 mwaka huu.

Zikiwa zimebaki siku tatu wanafunzi wa kidato cha sita kuanza mitihani yao mkuu huyo wa  wilaya amesema wanafunzi ambao wanatarajia kumaliza elimu yao ya kidato cha sita wanatakiwa kutambua jitihada za serikali katika kuufungua mkoa wa Kigoma kiuchumi na kuwa ni  fursa kwao.

Amesema miradi hiyo itatoa ajira kwa vijana ambao leo hii wanatarajia kumaliza kidato cha sita na kufanikiwa kwenda kwenye vyuo mbalimbali kuongeza ujuzi ambao utasaidia kuchochea maendeleo katika miradi ambayo serikali imewekeza na hivyo kuongeza pato la mkoa na Taifa kwa ujumla.

“ Nina waombea mfanye vizuri katika masomo yenu ni imani yangu walimu wamewafundisha vizuri hivyo mtulie na mfanye mtihani kwa weledi na umakini mkubwa Mungu atawaongoza  na nyinyi ndio tunaowatengemea huko baadae muwe wasimamizi wa miradi ambayo inaendelea kutekelezwa ndani ya mkoa wetu”

Katibu wa Mbunge Jimbo Kigoma Kaskazini  Mtemi Msaye akaeleza kuwa bado Taifa linahitaji wasomi ambao watakuwa viongozi wa badae kutokana na upungufu wa watumishi hivyo ipo haja ya kuendelea kuwaandaa vijana wazuri ambao watakuja kulisaidia taifa kimaendeleo na kiuchumi. 
  
Shule ya sekondari Nyarubanda ambayo inakidato cha kwanza hadi cha sita ina jumla ya wanafunzi 1003 ambayo imeelezwa kufanya vizuri zaidi katika mitihani ya kidato cha sita kwa kushika nafasi ya kwanza kimkoa lakini pia imeshawahi kushika nafasi ya 16 kitaifa.

Exavery Ndalikenye  ni Afisa Elimu Sekondari halmashauri ya wilaya ya Kigoma anaeleza kujivunia mafanikio ya shule hiyo kitaaluma ambapo kwa mwaka jana walifanikiwa kufuta matokeo ya daraja la tatu na malengo ya sasa yakiwa ni kupata daraja la kwanza pekee kwa matokeo ya kidato cha sita. 

Baadhi ya wanafunzi akiwemo Anord Simon, Anthon Kaspari na Majaliwa  Magazi wameeleza kujipanga vizuri katika mitihani yao ya kuhitimu kidato cha sita ambao utaanza Mei 2 na kumalizika Mei 8 ya mwaka huu.

Wamesema licha ya walimu kuwafundisha kwa jitihada zote lakini changamoto kadhaa zimekuwa kikwazo katika masomo yao ikiwemo ukosefu wa huduma ya maji ambayo hulazimika kuyafuata mbali na eneo la shule na hivyo kuchelewa kuanza kwa masomo yao ama muda wa kujisomea kukosekana.

Lakini pia bwalo wanalotumia kupata chakula na kufanyia vikao mbalimbali halitoshelezi kulingana na idadi kubwa ya wanafunzi pamoja na upungufu wa viti na meza ambavyo vinasababisha wao kutopata muda wa kusoma kwa pamoja na kulazimika kusoma kwa zamu.

Esnati Sumun ni mwalimu wa shule ya Nyarubanda ambaye anaeleza jitihada ambazo zimefanyika kuhakikisha huduma ya maji inapatikana ikiwa ni pamoja na kuchimba visima pamoja na kuweka mantanki mawili ya maji ambayo bado hayatoshelezi hususani wakati wa kipindi cha kiangazi.

Post a Comment

0 Comments