WALIMU WAKUU WA HALMASHAURI YA MJI WA KASULU KUTEMBELEA HIFADHI YA GOMBE.

Na Respice Swetu, Kasulu - Kigoma
Jumla ya walimu wakuu 72 wa shule za Msingi za Umma na binafsi zilizopo katika halmashauri ya Mji wa Kasulu, wanatarajia kufanya ziara ya siku mbili kwenye hifadhi ya wanyama ya Gombe na Makumbusho ya Dr. Livingstone.

Akizungumzia ziara hiyo, Mratibu wa safari ya walimu wakuu kwenda Gombe Mwl Wenseslaus Lugaya amesema, pamoja na kujifunza, ziara hiyo pia inakusudia kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuutangaza utalii na vivutio vya ndani.

Amesema kupitia ziara hiyo, walimu wakuu 72 hao watapata fursa ya kutembelea na kujionea mambo mbalimbali kwenye maeneo hayo.

Lugaya anayejulikana zaidi kwa jina la Ghadafi amesema,  kufanikiwa kwa ziara hiyo ni matokeo ya juhudi zilizofanyika kwa kuwahusisha wadau na wahisani mbalimbali.

"Tulipopata wazo la kufanya ziara hiyo tulimhusisha mkurugenzi wa mji wa Kasulu na wadau wengine na waliitika vizuri, nichukue nafasi hii kumshukuru sana mkurugenzi wetu kwa mchango wake na wafadhili wengine", amesema.

Pamoja na mkurugenzi wa Mji wa Kasulu kuchangia ziara hiyo, Ghadafi amewataja wadau wengine waliowezesha safari hiyo kuwa ni pamoja na mbunge wa Jimbo la Kasulu mjini Dr. Joyce Ndalichako na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Wilaya ya Kasulu.

Wengine kwa mujibu wa Ghadafi ni wafanya biashara wa mjini Kasulu, Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Kasulu, wamiliki wa shule binafsi na idara ya elimu Msingi ya halmashauri hiyo.

Aidha Ghadafi amefafanua pia kuwa kutokana na michango hiyo, gharama ya kufanyika kwa ziara hiyo kwa kila mmoja imepungua. 

"Nauli ya kwenda Kigoma na kurudi mmelipiwa, nauli ya kwenda Gombe na kurudi Kigoma mmelipiwa, gharama ya matembezi hifadhini mmelipiwa, gharama za chumba cha kulala mmelipiwa, kiingilio cha Livingstone mmelipiwa; mnatakiwa kulipa elfu 32 tu za chakula na vinywaji kwa kila mmoja kwa matumizi ya hizo siku mbili," amesema Ghadafi alipokuwa akiwahamasisha walimu kuchangamkia fursa hiyo.

Kufuatia hamasa hiyo, kundi la kwanza la Walimu litakalokuwa na walimu wakuu 50 litaondoka Jumamosi ya wiki hii huku safari ya kundi la pili itakayokuwa na walimu wakuu 22 likitarajiwa kuondoka mwishoni mwa mwezi ujao.  

Kufanyika kwa safari kimakundi kumetokana na maelekezo yaliyotolewa na uongozi wa hifadhi ya wanyama ya Gombe kwamba hawana uwezo wa kupokea "watalii" wanaozidi 50 kwa wakati mmoja.

Sambamba na kutembelea hifadhi ya wanyama ya Gombe na makumbusho ya Dr. Livingstone yaliyopo Ujiji Manispaa ya Kigoma, ziara hiyo pia itawafikisha walimu hao katika bandari ya Kigoma na kwenye uwanja wa ndege wa Kigoma.

Post a Comment

0 Comments