HALMASHAURI ZAKUMBUSHWA KUTENGA POSHO KWA WENYEVITI WA VIJIJI, MITAA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MBUNGE wa Vitimaalumu Neema Mwandabila (CCM), ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kutoa posho kwa Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji ili watekeleze majukumu yao kikamilifu.

Katika swali lake la nyongeza aliiomba serikali iwafikirie viongozi hao kwa kuwa wengine kutokana na kutokuwa na posho wamejitafutia njia nyingine za kujipatia kipato ikiwemo kuuza viwanja na kusababisha migogoro kwa wananchi.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Deogratius Ndejembi, alisema serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji katika kutoa huduma  kwa wananchi. 

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Sura ya 290, kila Halmashauri inatakiwa kuweka utaratibu wa kuwalipa posho, Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji kutoka katika vyanzo vya mapato vya ndani ya Halmashauri. 

Alisema serikali inaendelea kuzijengea uwezo Mamlaka za Serikali za Mitaa ili ziweze kubuni na kuimarisha vyanzo vya mapato pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha kwa kutumia mifumo ya kieletroniki ya kukusanya na kutumia fedha katika kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na matumizi mengineyo. 

“Kwa mujibu wa sheria posho hizi zinatakiwa zilipwe kutoka kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri,” alisema.

Katika swali la nyongeza la Neema pia alisema wenyeviti hao ndio wanaosimamia miradi ya serikali katika maeneo yao hivyo kwanini serikali haoni haja ya kuwalipa posho ya usimamizi.

Akijibu swali hilo, Ndejembi alieleza kuwa amepokea ushauri huo na kwamba serikali itaangalia endap bajeti itaruhusu.

Post a Comment

0 Comments