MAAGIZO YA RAIS SAMIA YAONGEZA UFANISI BANDARI YA KIGOMA

Na Adela Madyane, Kigoma.

Maelekezo ya kuboresha huduma katika bandari za ziwa Tanganyika yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa katika ziara yake mkoani Kigoma mnamo Oktoba 2022 yameanza kuzaa matunda kwa kupunguza changamoto ya urasimu na miundombinu mibovu katika bandari za mkoani humo.

Hayo yalibainishwa na wafanyabiashara na wasafirishaji wa mizigo kuelekea nchi za Congo na Burundi ambao wamekiri kuwepo kwa utaratibu mzuri wa kazi, shehena za mizigo zinashushwa kwa wakati na mizigo inasafirishwa bila kuwa na changamoto yoyote jambo ambalo linachochea maendeleo yao.

Tito Francis mfanyabiashara na msafirishaji wa chumvi na juisi kuelekea nchini Congo amesema mamlaka ya bandari pia imeanza kufanya ukarabati  wa miundombinu ambayo ilikuwa inaleta changamoto za usafirishaji wa mizigo kwa wakati na kwamba kwa sasa anaweza kufanya shughuli zake bila kipingamizi huku changamoto kubwa kuwa uchache wa mabehewa.

Kwa upande wa wakala wa usafirishaji wa shehena Julienne Mutabihirima ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Shegema iliyopo bandari ya Kibirizi amesema kutokana na kuboresha miundombinu ya ushushaji wa shehena sasa wanashusha tani 400 kwa masaa matatu jambo ambalo lilikuwa gumu miaka miwili iliyopita ambapo walishusha shehena za ujazo huo huo kwa siku tano.

Naye Mbaraka Said wakala wa meli za kusafirisha shehena alisema vifaa vya kisasa vilivyopo vimesaidia kushusha na kupakia mizigo kwa wakati na kwamba sasa mizigo inadhibitiwa tofauti na ilivyokuwa miaka miwili iliyopita na kuiomba serikali kuboresha usafiri wa reli ili kupunguza gharama zinazotumika kusafirisha mizigo kutumia barabara kutoka mkoani Kigoma kuelekeza nchi za Congo, Burundi na Zambia.

Aidha serikali ipo katika uboreshaji wa miundombinu ya bandari zilizopo mkoani Kigoma kutokana na umuhimu wake wa kufungua bandari ya Dar-es-Salaam ambayo asilimia 83 ya shehena inayotoka huko hupitia bandari za Kigoma kuelekea nchini Congo ambao ndio wateja wakubwa wakisafirisha bidhaa za chumvu, simenti, na bidhaa za chakula.

Akizungumza ufanisi wa wafanyakazi meneja wa bandari za ziwa Tanganyika Edward Mabula amekiri kuwa kuondolewa kwa baadhi ya wafanyakazi ni miongoni mwa sababu zilizoboresha huduma za bandari na kwamba wafanyakazi wameongezeka kutoka 54-67 huku nusu ya wafanyakazi wa zamani wakiwa wamebadilishwa.

Kwa upande wa ukarabati wa bandari za Kigoma, Mabula amesema kuwa serikali inatarajia kuanza kufanya ukarabati kwenye eneo la jengo la abiria na njia za kuingilia bandarini chini ya ufadhili wa JAICA kuanzia mwezi Septemba kwa kipindi cha miezi sita utakaogharimu dola milioni 21.

Amesema miongoni mwa miundombinu iliyoboreshwa na vifaa vilivyonunuliwa ili kuboresha utendaji kazi katika bandari ni pamoja na ujenzi wa kalakana mbili kubwa,vifaa vya kushushia mizigo na mashine mpya za umeme.

Mabula amekiri kuwa hatua hiyo ya kuboresha miundombinu imewezesha bandari kuingiza kiasi cha shilingi milioni 500 kwa mwezi na kuifanya bandari hiyo kuwa kinara kimapato ukilinganisha na bandari nyingine na kuwa na uwezo wa kuhudumia tani laki 5 za shehena kwa mwaka ili kukidhi mahitaji ya wateja wakubwa.

Ameongeza kuwa hadi sasa bandari ina uwezo wa kumudu shehena tani 130 kwa siku huku mzigo unaofika bandarini hapo kuwa tani 80-100 na kuiomba serikali kufanyia kazi changamoto ya mabehewa ambayo yanayohitajika kukidhi haja ya bandari ili kupunguza adha ya usafiri wa wateja waliopo.

“Ili kupunguza changamoto za usafirishaji bandari inahitaji uwepo wa mabehewa 50, lakini sasa yapo mabehewa 8-10 yanayofika mkoani Kigoma, hali hii inaleta changamoto kwa wasafirishaji kwakuwa mizigo inachelewa kufika, huchukua kati siku 30 hadi 45 kufikisha mzigo Kigoma na unafika kidogo kidogo jambo linaloleta ugumu kwa wafanyabishara kukodi meli” Alisema Mabula.

Akizungumzia changamoto ya mabehewa mkuu wa kituo cha reli Kigoma Ally Shamte amesema serikali ipo kwenye mpango wa kukarabati mabehewa 600 kwaajili ya kuja kuondoa changamoto iliyopo na kuboesha uchumi wa wafanyabiashara

Post a Comment

0 Comments