MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI YATAKIWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE.

Na Respice Swetu, Kasulu
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma Kanali Isaac Mwakisu, amezitaka asasi na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi katika Wilaya hiyo, kutekeleza majukumu yao.

Akifungua kikao kazi cha mwaka cha viongozi wa mashirika hayo kilichofanyika kwenye ukumbi wa boma mjini Kasulu Kanali Mwakisu amesema, kwa muda ambao amekuwepo katika Wilaya ya Kasulu, amebaini kuwepo kwa asasi na mashirika mengi huku mengine yakiwa hayafanyi kazi.

"Kuna mashirika mengi katika Wilaya ya Kasulu lakini kinachofanyika hakilingani na wingi wa mashirika yaliyopo, mimi niko tayari kubaki na mashirika machache yanayofanya kazi kuliko kuwa na wingi wa mashirika yasiyofanya kazi" amesema.

Akitoa mfano wa mashirika yanayofanya kazi, Mwakisu amesema shirika la Water Mission linalotoa huduma za maji kuwa ni miongoni mwa mashirika yanayofanya vizuri.

"Water Mission wanafanya kazi nzuri sana, wamejenga miradi mingi ya maji na huwa wanakuja kunipa taarifa ya miradi yao na kunichukua kwenda kuiona",  amesema.

Aidha Kanali Mwakisu amewataka viongozi wa asasi na mashirika yasiyo ya kiserikali ambao hawajafika ofisini kwake wafanye hivyo ikiwa ni pamoja na kumpa taarifa ya asasi zao, mahali walipo na shughuli wanazotekeleza.

"Najua Watanzania tuko vizuri sana katika kuandika na kufanya michakato, mimi sijawahi kufundishwa michakato, nimefundishwa kazi na kutoa matokeo", amesema.

Ili kuhakikisha utendaji kazi wa mashirika na asasi hizo unakuwa endelevu, Mwakisu amewaelekeza viongozi wa mashirika hayo kuweka mikakati ya kuziendesha taasisi hizo kwa kujitegemea badala ya kutegemea wafadhili.

Hata hivyo mkuu huyo wa Wilaya amekitumia kikao hicho kukemea vitendo vya ushoga na usagaji na kuwataka viongozi wa mashirika hayo kusaidiana na serikali kupiga vita suala hilo.

 "Watanzania tuna maadili na utamaduni wetu, na endapo nitagundua eneo lolote kwenye Wilaya yangu kuna viashiria vya kuwepo vitendo hivyo nitachukua hatua kali", ameonya.

Pamoja na kupokea taarifa za utendaji kazi kutoka kwa mashirika na asasi mbalimbali zilizopo wilayani Kasulu, kikao hicho pia kilipokea taarifa za miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye halmashauri pacha ya Mji na Wilaya ya Kasulu zinazonufaika na mashirika hayo. 

Post a Comment

0 Comments