WANANCHI KIGOMA WATAKIWA KUDHIBITI WIZI KATIKA MIRADI YA BARABARA

Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewataka wakazi katika maeneo yote ambayo Serikali inatekeleza Miradi ya Ujenzi wa Barabara mkoani humo, kuvisaidia vyombo vya usalama kudhibiti wizi wa Mafuta, vipuri vya Magari na vifaa vya ujenzi vinavyotumika katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Kauli hiyo ameitoa Mei 11, 2023 alipofanya ziara ya kikazi katika wilaya za Buhigwe na Kasulu kwa lengo la kukagua Maendeleo ya utekelezaji wa Miradi ya Ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami katika wilaya hizo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake kimkoa na kusisitiza kuwa, kitendo cha wananchi kutotoa taarifa za kufichua ubadhilifu ni sehemu ya wao kushiriki katika uhujumu uchumi wa Nchi. 

Amesema katika maeneo mengi inakotekelezwa miradi ya Ujenzi wa barabara mkoani humo, tabia ya wizi wa vitendea kazi imekuwa ni jambo la kawaida na jamii haichukui hatua zozote kwa lengo la kuwadhibiti wahusika wa vitendo hivyo.

‘’Mnapoendelea kutochukua hatua na kuviona vitendo hivyo ni halali, mkumbuke kuwa fedha wanazopewa wakandarasi kutekeleza miradi hii ya barabara zinatokana na kodi zenu hivyo mnaporuhusu wizi ufanyike mtakaopata hasara ni ninyi wenyewe kutokana na miradi kutokukamilika kwa wakati au kutekelezwa chini ya kiwango’’ amesema Andengenye. 

Kupitia ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa amekagua ujenzi wa barabara ya hospitali ya Buhigwe yenye Urefu wa Km. 3.5, Kasumo hadi Muyama Km. 12.5, Barabara ya Mji Kasulu Km.1, pamoja na ujenzi wa mfereji wa maji wenye urefu wa Km. 2. 

Aidha Andengenye amekagua ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika eneo la Makao makuu ya Halmashauri ya wilaya ya Kasulu zenye jumla ya urefu wa kilomita 1.5 na kuhitimisha ziara yake katika maeneo hayo kwa kuwasisitiza wakandarasi kusimamia ubora na kuzingatia muda wa mikataba katika utekelezaji wa miadi.

Post a Comment

0 Comments