WADAU MKOANI KIGOMA WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUTOKOMEZA TATIZO LA UDUMAVU

Na Emmanuel Matinde, Kigoma
Imeelezwa kuwa licha ya mkoa wa Kigoma kuonekana kupunguza tatizo la udumavu kutoka asilimia 42.3% hadi kufikia asilimia 27.1% kulingana na takwimu za Tanzania Demographic and Health Survey TDHS za mwaka 2022, bado ipo haja ya wadau wote kushirikiana ili kutokomeza kabisa tatizo hilo.

Ili kuhakikisha kuwa tatizo la udumavu linaendelea kupungua Kamati Jumuishi ya Lishe mkoa wa Kigoma imekutana ili kupokea taarifa ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi mwaka 2023, kujadiliana na kuweka mikakati ya kusimamia viashiria.

Katika kikao hicho cha robo ya tatu mwaka 2023, Afisa Lishe Mkoa wa Kigoma James Ngalaba, amezitaka idara husika zinapotekeleza afua za lishe ziingize takwimu kwenye mfumo ili kufahamu kila hatua inayopigwa katika masuala mtambuka ya afya, elimu, kilimo, maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii.

Wakati tayari serikali ikiwa imeelekeza shule zote kutoa chakula kwa wanafunzi; ni shule 91 tu za msingi watoto wanakunywa uji shuleni na shule 171 wanakula chakula kati ya shule 712 za msingi zilizoko mkoani Kigoma,  ,huku shule za sekondari 15 watoto wanakunywa uji na shule 70 wanakula chakula kati ya shule za sekondari 238 zilizoko mkoani Kigoma.

Changamoto inatajwa kuwa ni ushirikiano mdogo kutoka kwa wazazi ambapo Kaimu Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Kigoma Viwanda na Uwekezaji Deogratius Sangu, ambaye alikuwa Mmwenyekiti wa kikao hicho, amehimiza wazazi kuchangia chakula.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Lishe mkoa wa Kigoma Pascal Hamenya, ametoa ushauri kwa shule zote kuwa na mpango wa kilimo kwa ajili ya kulima viazi lishe ambavyo amesema vitasaidia sana suala la lishe mashuleni.

Post a Comment

0 Comments