WAFANYABIASHARA KIGOMA WATAKIWA KUZIGATIA MATUMIZI SAHIHI YA VIPIMO


Na Tryphone Odace, Kigoma.

Wafanyabiashara Mkoani Kigoma wametakiwa kuzingatia  matumizi  sahihi ya vipimo kwenye mfumo wa usambazaji na uzalishaji wa chakula  kutokana na kwamba baadhi yao wamekuwa wakitumia vipimo ambavyo vinawanyonya wakulima.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya Kasulu Kanali Isac Mwakisu kwa niaba Mkuu wa Mkoa wa Kigoma katika maadhimisho ya siku ya vipimo duniani ambapo amesema wakulima wamekuwa wakitumia vipimo ambavyo havikidhi vigezo na hivyo kuwa chanzo cha unyonyaji wa wakulima.

Naye Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Nchini Bi. Stella Kahwa amesema watahakikisha wanaendelea kufanya ukaguzi wa vipimo ambavyo vinatumika ili kuhakikisha wananchi hawatumi vipimo visivyokidhi viwango vya kimataifa.

Hafla hiyo ya siku ya vipimo duniani ambayo kitaifa imeadhimishwa Mkoani Kigoma imeambatana na Wakala wa Vipimo kugawa vipimo kwa wakulima na wafanyabiashara ambavyo vimekaguliwa na wakala wa vipimo ambapo baadhi ya wakulima wamesema vipimo hivyo vitawasaidia kuondokana na unyonyaji kutoka kwa wafanyabiashara ambao wamekuwa wakitumia mabidoo kupima bidhaa hususani mafuta ya mawese.

Aidha Kanali Mwakisu amewaagiza Maafisa biashara na wakurugenzi kwa kila halmashauri wanafanya ukaguzi ili kuhakikisha vipimo ambavyo havikidhi vigezo havitumiki.

Siku hii ya vipimo duniani  ilianzishwa mwaka 1875 Nchini ufaransa ambapo zaidi ya mataifa 17 yalikutana na kukubaliana kuweka kipimo kitakachikubalika kama mlingano wa kipimo cha bidhaa ili kusaidia wazalishaji hasa wakulima kuepuka kutumia vipimo vikubwa ambavyo vinatajwa kuzidi ujazo unaotakiwa.

Maadhimisho ya siku ya vipimo mwaka huu yameenda sambamba na kaulimbiu imesemayo ‘vipimo katika kuwezesha mfumo wa usambazaji wa chakula duniani’.

Post a Comment

0 Comments