Mkuu wa shirika hilo ofisi ya Kasulu Bw. Ben Diallo ameyasema hayo wakati wa uhamasishaji wakimbizi wa Burundi katika kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu Mkoani Kigoma na kuongeza kuwa ili kuongeza kasi ya wakimbizi kurejea kwa hiari mkutano wa pande tatu ambao umefanyika mapema mwezi huu mkoa wa Gitega nchini Burundi umeazimia kuongeza fedha kwa kila mkimbizi.
Amesema mkutano huo uliozihusisha nchi za Tanzania, Burundi na UNHCR umeongeza kiwango kutoka dola za kimarekani 75 kwa mtoto na dola 150 kwa mtu mzima na kufikia dola 200 kwa kila mkimbizi.
Makubaliano hayo yanakwenda sambamba na ongezeko la uzito wa mizigo inayobebwa na wakimbizi pamoja na Serikali ya Burundi kuweka mazingira wezeshi kwa wakimbizi wanaorudi ili waweze kupokelewa na kupewa maeneo ya kuishi sambamba na kujumuisha watoto katika elimu wanayosoma kwa sasa katika kambi za wakimbizi mkoani kigoma.
Diallo ameongeza kuwa kwa sasa maafisa kutoka mashirika yanayofanya kazi ya kuhudumia wakimbizi yatafanya kazi ya uhamasishaji kwa pamoja ili kuhakikisha wakimbizi wote wa nchi hiyo wanarudi Burundi.
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Sudi Mwakibasi akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kuwahamasisha na kuwapa mrejesho wa mkutano huo kambini Nyarugusu amesema hatua hii ya motisha ni hatua ya pili katika utaratibu wa urejeshaji wakimbizi ikitanguliwa na urejeshaji wa hiari na sasa wanatoa motisha na hatua inayofuata ni ufungaji wa kambi.
Amesema mpango huo ni wa miezi sita ambapo wakimbizi zaidi ya elfu arobaini na tisa wanatarajiwa kuandikishwa kwa hiari na kurejeshwa kabla Serikali na UNHCR hawajafanya maamuzi mengine juu ya wakimbizi hao.
0 Comments