WAKULIMA WA ZAO LA PAMBA KIGOMA WAOMBA MAREKEBISHO YA BEI


Na Adela Madyane, Kigoma

Wakulima wa pamba wilayani Kasulu mkoani Kigoma  wameiomba serikali kufanya marekebisho ya bei elekezi ya zao hilo iliyotangazwa kuanza kutumika kwa mwaka wa fedha 2023-2024.


Wamesema serikali imetangaza bei ya kuanzia katika gulio la ununuzi wa pamba kuwa ni 1060 kwa kilo moja bei ambayo imeshuka kwa sh 500 kutoka 1560 iliyotumika kununua kila moja ya pamba kwa mwaka wa 2022-2023.


Akizungumzia hilo Mariam James mkulima wa zao la pamba amesema bei elekezi iliyotangazwa kutumika haitaleta hamasa zaidi ya kilimo cha zao hilo kwakuwa wakulima wengi watashindwa kurudisha gharama za kilimo  na kujikuta wakipata hasara na kushindwa kumudu familia zao vema.


Akizindua msimu wa ununuzi wa pamba kwa mwaka huo mkurungenzi mkuu wa bodi ya pamba Tanzania Marko Mtunga amesema Tanzania ni miongoni kwa nchi zinazozalisha Kiwango kidogo cha pamba ambapo huzaliasha kwa asilimia 0.2% kwa mwaka hivyo haina nguvu ya kupanga bei na kulazimika kupokea bei inayojitokeza katika soko la dunia ambapo kwa mwaka huu bei katika soko hilo imeporomoka tofauti na mwaka jana.


“Kimsingi nchi yetu haina ushindani wa soko katika zao la pamba kutokana na uzalishaji mdogo wa zao  na  sasa tumekuwa watu wakupokea  maelekezo ya bei ambayo yanakuja kutoka sokoni”alisema Mtunga.


Mtunga amesema katika kukabiliana na hali hiyo serikali imetoa ruzku kwa zao la pamba ambapo mkulima hatowajibika kulipia gharama za pembejeo ili pesa anayopata kwa kuuza pamba iwe mali yake tofauti na ilivyokuwa mwaka jana


Mtunga amewatoa hofu wananchi kuwa bei iliyotangazwa ni ya kianzio na kwamba itaendelea kupanda kadri siku zinavyoendelea  


Zaidi Mtunga amewataka wakulima wa pamba nchini kuendelea kufanya juhudi katika kilimo cha zao hilo kwa kutumia kanuni za kilimo bora ili wafikie uzalishaji wa kilo Elfu mbili kwa hekari kiwango kitakachosaidia kuwapatia fedha nyingi kwa bei hiyo ndogo tofauti na uzalishaji wa sasa ambapo wengi huzalisha kilo mia mbili kwa hekari 


Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Kasulu Isaac Mwakisu ameitaka bodi ya pamba kuboresha miundombinu ya uzalishaji wa zao hilo kwa kuwapatia wakulima elimu ya kisasa pamoja na vitendea kazi  ili kuepuka ukulima  wa kutumia jembe la mkono na kuhakikisha mkulima anapatiwa sitahiki zake ili kumuinua kiuchumi

Post a Comment

0 Comments